Ligi Kuu

Kakolanya ayamaliza na Fountain Gate

DAR ES SALAAM: NDOA ya kipa wa timu ya Fountain Gate FC, Beno Kakolanya na uongozi wa klabu hiyo imevunjika rasmi na kumpa baraka nyanda huyo katika changamoto nyingine kwa msimu ujao.

Kakolanya amewaaga waajiri wake wa zamani Fountain Gate baada ya kuwatumikia kwa msimu mmoja wakati alisaini mkataba wa miaka miwili unaotarajiwa kufikia tamati 2026 inadaiwa huenda msimu ujao akawa sehemu ya kikosi cha Namungo FC.

Kipa huyo aliingia kwenye mgogoro na timu hiyo baada ya kudaiwa kuhujumu timu hiyo kwa kutoroka kambini wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya mchezo dhidi ya Yanga na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Akizungumza na Spotileo, Kakolanya amekiri kuachana na waaajiriwa wake hao baada ya kumaliza pande zote mbili bila ya kujadiliwa katika kamati ya hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

“Kila mmoja tulipeleka malalamiko TFF na jana ilikuwa kusikilizwa lakini kabla hatujaanza kusikilizwa viongozi wa Fountain walitaka jambo hilo tumalizane kwa kukubali kunipa barua ya kuachana na kunipa baraka zote,” amesema Kakolanya.

Naye Ofisa habari wa timu hiyo, Issa Mbuzi alikiri kuwepo kwa mazungumzo hayo na kuafikiana muafaka na kipa huyo kwa kuachana salama na kumpa baraka za anapokwenda katika changamoto nyingine.

“Ni kweli Beno alikuwa na mkataba wa miaka miwili na kuutumikia mmoja na 2026 unafikia ukingoni, lakini kwa sababu tulikaa pande zote mbili na kumaliza vizuri, kupewa baraka zote anapokwenda ,” amesema Ofisa habari huyo.

Related Articles

Back to top button