Burudani

Shetta apongeza majukwaa ya ubunifu

DAR ES SALAAM: MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma ‘Shetta’, amesema majukwaa ya ubunifu kama Her Creative Spark yana mchango mkubwa katika kukuza sekta ya ubunifu nchini kwa kuwapa vijana fursa ya kujifunza na kuonesha vipaji vyao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Shetta amewapongeza waandaaji wa tukio hilo kwa juhudi zao za kuibua na kuendeleza vipaji, ameeleza kuwa mafunzo maalum yaliyotolewa kabla ya tukio kuu yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea washiriki ujuzi wa vitendo.

“Majukwaa kama haya yana mchango mkubwa katika kukuza sekta ya ubunifu kwa kuwapa vijana nafasi ya kujifunza na kuonesha uwezo wao,” amesema Shetta

Ameongeza kuwa majukwaa hayo huwasaidia vijana kuunganishwa na wadau mbalimbali wa tasnia, jambo linalofungua milango ya fursa na maendeleo ya taaluma zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa We Media, Winnie Nzunda, amesema kuwa kuanzishwa kwa Her Creative Spark kulitokana na changamoto ya ushiriki mdogo wa wanawake katika sekta ya filamu na uzalishaji wa maudhui.

“Tulibaini kuna pengo kubwa la ushiriki wa wanawake katika tasnia hii, hivyo tukaanzisha jukwaa hili ili kutoa mafunzo, mwongozo na fursa kwa wanawake kujitokeza na kuonesha vipaji vyao,” amesema Nzunda.

Amefafanua kuwa kupitia warsha na tukio hilo, washiriki walipata ujuzi wa vitendo pamoja na nafasi ya kuwasilisha kazi zao mbele ya wadau wa tasnia, hatua inayosaidia kukuza taaluma zao.

Tukio hilo liliwakutanisha wabunifu chipukizi, wataalamu wa tasnia pamoja na wadau mbalimbali, na lilijumuisha maonyesho ya kazi za ubunifu, mijadala ya kitaalamu, pamoja na utoaji wa vyeti kwa washiriki.

Aidha, Shetta alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya vitendo yaliyotolewa kabla ya tukio, akieleza kuwa ni msingi muhimu katika kujenga taaluma endelevu kwa vijana katika sekta ya ubunifu.

Tukio la Her Creative Spark lilidhaminiwa na Serengeti Premium Lite kupitia kampeni yake ya “Lite Your Imagination”, inayolenga kuibua na kuhamasisha vipaji vipya vya ubunifu nchini.

Kwa sasa, Her Creative Spark inaendelea kujidhihirisha kama jukwaa muhimu katika kukuza ubunifu, kuunganisha vipaji na fursa, pamoja na kuhamasisha kizazi kipya cha wabunifu nchini Tanzania.

Related Articles

Back to top button