
KAMA unapenda kutazama fi lamu za kijasusi zenye mapigano ya kutisha basi fi lamu ya Salt iliyotoka miaka 13 iliyopita ni kwa ajili yako. Bila shaka uigizaji mzuri wa Angelina Jolie, Liev Schreiber pamoja na August Diehl umefanya fi lamu hii iwe bora sana.
Sasa tusipoteze muda! Filamu hii inamhusu mwanadada Evelyne Salt, ajenti wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA, ambaye anasingiziwa kuwa ni mpelelezi kutoka Urusi na hivyo
anatakiwa kutumia ujuzi wa kijasusi alio nao kuepuka mikono ya CIA.
Evelyne Salt ni agent hatari wa CIA ambaye anafanya kazi na Ted Winter pamoja na mpelelezi mwingine hatari, Darryl Peabody.
Kabla ya sakata hili, Evelyne Salt alikuwa amefungwa gerezani nchini Korea Kaskazini akituhumiwa kuwa jasusi wa Marekani kisha akatolewa kwa njia ya mabadilishano ya wafungwa.
Miaka miwili baadaye Evelyne Salt akiwa na Ted Winter, anaitwa kumfanyia mahojiano mkimbizi mmoja kutoka Urusi, Oleg Vasilyevich Orlov ambaye anakiri kwamba, shirika la
kijasusi la Urusi limepenyeza wapelelezi wake ndani ya CIA ambao wana lengo la kumuua Rais wa Urusi, Boris Matveyev, ambaye yupo nchini Marekani kuhudhuria mazishi ya Makamu wa Rais wa Marekani.
Inasemwa kuwa mpango huu wa mauaji unafanywa na wapelelezi kutokea Urusi na mmojawao ni yeye mwanadada Evelyne Salt, ambaye anatumia utambulisho wa ‘Ajenti KA-12’.
Mara moja baada ya taarifa hiyo kuvuja kutoka kwa Orlov inasemwa kuwa Evelyne Salt ni msaliti wa CIA, Darryl Peabody anaamuru Salt akamatwe ili awekwe chini ya ulinzi wa CIA, lakini wanachelewa kwani Salt anatoroka kwa kujua kuwa yuko hatarini kuuawa na CIA.
Vasilyevich Olov pia anatoroka baada ya kuua wapelelezi wawili. Baada ya kutoroka, Evelyne Salt anakwenda kumtafuta mumewe, Mike Krause, ila anakuta ameshatekwa na
watu wasiojulikana.
Evelyne Salt anaamua kujipanga tayari kwa lolote. Tunaoneshwa kuwa ni kweli Evelyne Salt amezaliwa nchini Urusi na ni ajenti wa Urusi kwa maana ya kwamba ni mpelelezi wa muda mrefu wa nchi hiyo.
JASUSI WA URUSI ALIYEITIKISA MAREKANI
Baada ya muda kujipanga tayari kwa lolote, Evelyne Salt anaenda kwenye msiba wa Makamu wa Rais wa Marekani na anafanikiwa kumuua Rais wa Urusi aliyehudhuria msiba huo kisha anatoroka baada ya kuwakimbia polisi.
Baadaye Salt anakutana na Orlov ambaye inafahamika kuwa ni mpelelezi wa Urusi na ndiye ambaye alimteka Mike, mume wa Evelyne Salt. Mbele ya macho ya Salt, Orlov anamuua Mike, mume wa Salt ili kumpima imani.
Evelyne Salt anajizuia ila anashindwa kwani anaishia kumuua Orlov na wapelelezi wote wa Urusi waliokuwepo kwenye boti hiyo kama kisasi cha mauaji ya mume wake.
Baada ya kumalizana na Orlov, Evelyne Salt anaelekea Ikulu ya Marekani ambako anakuta hali ni tofauti kabisa na alivyodhani, huko anafahamu kuwa mpelelezi mwenzake na rafiki yake, Ted Winter, ambaye alifahamika kuwa mpelelezi wa CIA kumbe ni ajenti kutoka Urusi na jina lake halisi ni Nikolai Tarkovsky.
Lengo la Ted Winter ni kutaka kuanzisha vita ya kinyuklia na amelenga kuishambulia miji ya Mecca na Tehran ili kuibua hasira za Waislamu dhidi ya nchi ya Marekani.
Ted Winter ameua walinzi wote wa Rais wa Marekani na anamwacha Rais akiwa hai ili ampe ‘password’ za kufyatua nyuklia na hapo ndipo Evelyne Salt anatokea na mapigano makubwa yanayokea kati ya Salt na Winter na hatimaye Salt anamuua Winter, kisha anamsaidia Rais wa Marekani na kuepusha vita ya nyuklia.
Baadaye Salt anakamatwa na wanausalama wa Marekani na anapandishwa kwenye helikopta na baada ya Darryl Peabody kuguswa na stori ya Salt anaamua kumruhusu awe huru kwa kumuachia ajitumbukize kwenye mto Potomac…
Filamu hii ilipata umaarufu mkubwa sana ilipoingia sokoni mwaka 2010 kiasi cha kutajwa kwenye Tuzo za 83 za Oscar huko nchini Marekani. Ni filamu ya dakika 104, ikiwa imeandikwa na Kurt Wimmer na kuongozwa na Phillip Noyce.
Filamu hii imetengenezwa kwa bajeti ya Dola za Marekani kati ya milioni 110 na 130, na imeingiza pato la Dola milioni 293.5 kupitia maonesho ya filamu.
0755 666964 au bjhiluka@ yahoo.com