
DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Yanga, Max Nzengeli, amesema kucheza kwa muda mrefu na kutumia nguvu nyingi uwanjani ni miongoni mwa sababu zinazoweza kufanya kiwango cha mchezaji kupungua na kilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.
Nzengeli amesema ni jambo la kawaida kwa mchezaji ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara kwa dakika nyingi kushindwa kuwa na ubora ule ule kila wakati, ingawa bado anaendelea kupambana na kujitahidi kuisaidia timu yake.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kiwango chake kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, Nzengeli amesema pamoja na changamoto hiyo, bado ana ari ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii kila anapopewa nafasi ya kucheza.
“Nimecheza kwa muda mrefu sana, kiwango hakiwezi kuwa kama nilivyoanza. Unacheza dakika 90 uwanjani, lakini napambana na najitahidi,” amesema Nzengeli.
Amefafanua kuwa hata katika maisha ya kawaida ya kazi, mtu anapofanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika vya kutosha kuna wakati ufanisi unaweza kushuka.
Pamoja na hali hiyo, kiungo huyo ameweka wazi kuwa bado anaendelea kupambana ili kurejea katika kiwango chake bora na kuendelea kutoa mchango muhimu ndani ya kikosi cha Yanga kinachoendelea na harakati za mashindano ya ndani.



