DK Mwigulu ampeleka Feitoto Simba
WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ni kama amewasha taa ya kijani kwa Simba ikiwa wanataka kumsajili kiungo Feisal Salum, ‘Feitoto’ baada ya waziri huyo kuandika ujumbe wa kumshauri Feitoto kumaliza mitaa ya timu za Dar es Salaam ikiwa ni Chamazi, Jangwani na Msimbazi.
Kupitia ukurasa wa mtandao wake wa Instagram, Mwigulu amempongeza nyota huyo kwa kufunga bao la kusawazisha katika mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Guinea Septemba 10 nchini Ivory Coast.
Waziri huyo ameandika, “ Mwanangu Buana, ulifunga goli muhimu sana katika mechi ya muhimu sana jana, anyway hii ni kawaida yako ndio ulifanya ukiwa mitaa ya Jangwani.
Ndivyo unaendelea na Chamazi, mwanangu kwani vipi ukimaliza kabisa mitaa ya Dar es Salaam, yaani Msimbazi kabla ya kuja Singida? Si baba kasema,” amemaliza hivyo.
Fei Toto amekuwa akihusishwa na kutakiwa na Simba na nyota huyo amekiri kuwa kama viongozi wa klabu hiyo watafuata taratibu yeye hana pingamizi maana mpira ni kazi yake, kauli ya Mwigulu inaamsha upya joto la Feitoto kutua Simba.