Ligi Kuu

Jeuri ya Yanga kwa Simba bado ipo

...presha ya ubingwa yazidi kupanda

DAR ES SALAAM: LICHA ya Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kwa muda kupisha ratiba ya timu ya taifa inayoshiriki michezo ya FIFA Series nchini Rwanda, vita ya ubingwa baina ya watani wa jadi Yanga na Simba imeendelea kuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.

Hadi ligi iliposimama, Yanga bado imeendelea kuonyesha jeuri yake juu ya watani wao Simba, kwa kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza michezo 16.

Ubora huo wa Yanga umeendelea kuonekana licha ya timu hiyo kupata sare tatu mfululizo katika mechi zake za karibuni, jambo ambalo lingeweza kuwapa nafasi wapinzani wao kusogea karibu zaidi.

Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya Simba wanaoshika nafasi ya pili, ingawa wekundu hao wa Msimbazi bado wana michezo miwili ya viporo mkononi, hali inayofanya mbio za ubingwa kuwa wazi zaidi.

Ikiwa Simba watafanikiwa kushinda mechi hizo mbili za viporo, basi pengo hilo litapungua na kubaki pointi moja tu, jambo litakaloongeza presha kubwa kwa mabingwa hao watetezi.

Mbali na ubora wao kwenye msimamo, Yanga pia wameonesha uimara mkubwa msimu huu kwa kuwa bado hawajapoteza mchezo wowote, wakibaki miongoni mwa timu chache zenye rekodi hiyo, sambamba na Azam FC. Kwa upande wa Simba, wao tayari wameonja kichapo cha mchezo mmoja.

Katika safu ya ushambuliaji, Yanga pia wameonekana kuwa na makali zaidi baada ya kufunga mabao 32, idadi kubwa zaidi kuliko Simba ambao mpaka sasa wamefunga mabao 24.

Hata hivyo, pamoja na takwimu hizo kuipa Yanga faida ya kisaikolojia, kasi ya Simba katika mechi za hivi karibuni imeanza kuwatisha wapinzani wao.

Wekundu hao wameonesha kiwango cha juu na muendelezo mzuri, hali inayowafanya mashabiki wao kuamini kuwa wana nafasi halisi ya kuusaka ubingwa msimu huu.

Kwa upande mwingine, Yanga wanaonekana kuingia katika kipindi kigumu zaidi kadri msimu unavyosonga mbele, hasa kutokana na changamoto ya majeruhi ya baadhi ya wachezaji muhimu, jambo linaloweza kuathiri uimara wao katika mbio hizi za mwisho.

Hali hiyo inafanya ushindani wa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kuendelea kuwa wa kusisimua na wenye mvutano mkubwa, huku kila timu ikionekana kuwa na sababu ya kuamini inaweza kutwaa taji.
Kwa sasa, ni mapema mno kumtaja bingwa.

Yanga wanaonekana kuwa na dhamira ya kutetea taji lao, lakini Simba nao wanaonesha wazi kuwa safari hii wameamua kurudisha heshima ya ubingwa Msimbazi baada ya kuukosa kwa muda.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona nani atakayekuwa na nguvu, utulivu na muendelezo bora zaidi ligi itakaporejea kwa sababu kwa mwendo huu, vita ya ubingwa bado iko wazi kabisa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button