Ligi Kuu

Yanga, Azam zatambiana, mechi ya presha, kisasi

ZANZIBAR: YANGA na Azam zinakutana tena kesho katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.

Timu hizo zimetoka kukutana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho juzi ambapo Yanga ilipoteza mabao 3-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo muhimu wa kesho dhidi ya Azam FC huku akisisitiza kuwa kila mechi iliyobaki ni sawa na fainali katika harakati za kutetea ubingwa.

Moallin amesema maandalizi ya timu yamekwenda vizuri na habari njema ni kwamba hakuna majeruhi wakubwa, jambo linalompa uhakika wa kuwa na kikosi kamili kwa mchezo huo.

“Maandalizi yanaendelea vizuri. Kwa bahati nzuri hatuna majeruhi wakubwa na wachezaji wote wako tayari kwa mchezo muhimu wa kesho. Kila mchezo uliobaki ni fainali kwetu kwa sababu lengo letu ni kutetea ubingwa,” alisema.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Azam FC Kassim Liogope amesema amesema kikosi chake kimejipanga vizuri kuelekea mchezo huo muhimu dhidi ya Yanga, akieleza kuwa ni mechi yenye ushindani mkubwa kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri baada ya kukutana mara kadhaa msimu huu.

Amesema Azam inaiheshimu Yanga kutokana na ubora wa kikosi chake, uzoefu wa wachezaji na uwezo wa benchi la ufundi, lakini amesisitiza kuwa timu yake iko tayari kupambana kwa ajili ya ushindi.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu tumekutana mara nyingi msimu huu. Tunaiheshimu Yanga, wana wachezaji wenye uzoefu na kocha mzuri. Hizi ni mechi zenye ushindani mkubwa, lakini pia ni mechi ambazo sisi Azam tunazipenda,” amesema.

Kocha huyo aliongeza kuwa wamepata muda wa kutosha kujiandaa, kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita na kuhakikisha kila mchezaji yuko tayari kwa changamoto ya kesho.

Pia, amewataka mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo, akisisitiza kuwa Zanzibar imekuwa ngome muhimu ya mashabiki wa klabu hiyo.

 

Related Articles

Back to top button