Filamu

Wasanii watakiwa kutangaza utalii kupitia filamu

DAR ES SALAAM: WASANII wa filamu nchini wametakiwa kuhakikisha kazi wanazozalisha zinatumika kama jukwaa la kutangaza vivutio vya utalii, hatua itakayosaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania.

Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Gervas Kasiga, wakati wa hafla ya ugawaji tuzo na vyeti kwa wanafunzi walioshinda shindano la Guardians of the Peak University Challenge.

Amesema miradi ya aina hiyo ina mchango mkubwa si tu katika kukuza sekta ya filamu, bali pia katika kulinda mazingira, kukuza utalii na kuimarisha uchumi wa taifa.

Dk Kasiga ameipongeza Ram Films Company kwa juhudi zake za kuwaunganisha vijana, mazingira na utalii kupitia sanaa ya filamu, akieleza kuwa mradi wa Guardians of the Peak ni mfano bora wa namna filamu inavyoweza kuchangia maendeleo katika nyanja mbalimbali.

“Mradi huu unaonesha wazi jinsi filamu inavyoweza kusaidia katika uhifadhi wa mazingira, kukuza utalii, uwezeshaji wa vijana, matumizi ya nishati safi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na mataifa mengine kama China,” amesema Dkt Kasiga.

Ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa sekta ya filamu katika kuitangaza nchi kimataifa, hasa kwa kuonesha uzuri wa vivutio vya asili, urithi wa kitamaduni na mandhari ya kipekee.

Kutokana na hilo, amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo kwa kurahisisha upatikanaji wa vibali vya utengenezaji wa filamu pamoja na kuhamasisha ushirikiano kati ya wazalishaji wa ndani na wa kimataifa.

Kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), juhudi zinaendelea kufanywa kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo bora ya upigaji wa filamu duniani.

Amesema lengo kuu ni kuhakikisha filamu zinazozalishwa nchini zinatumika pia kuonesha vivutio vya utalii na hivyo kuongeza idadi ya wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Akizungumzia mradi wa Guardians of the Peak, Dkt. Kasiga amesema unatoa mfano halisi wa jinsi filamu inavyoweza kuitangaza Tanzania kupitia vivutio kama Mlima Kilimanjaro na kuvutia watalii.

Aidha, amefurahishwa na ushiriki mkubwa wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika mradi huo, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa vijana kujifunza, kubuni na kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira na utalii.

Pia amewapongeza wadau mbalimbali wanaounga mkono mradi huo wakiwemo Zara Tanzania Adventures, Meticulous, COSOTA, Digi Farm, Skyward Airline, Red Gold Tanzania, Titan Watches Tanzania pamoja na EACLC.

Ametoa wito kwa sekta binafsi na wadau wengine kuendelea kuunga mkono miradi kama hiyo, akisisitiza kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

“Kwa pamoja tunaweza kuifanya Guardians of the Peak kuwa jukwaa kubwa la kimataifa litakaloiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee duniani kupitia filamu,” amesema Dk Kasiga.

Related Articles

Back to top button