Filamu

Saving Private Ryan

VITA imepamba moto, ni katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia (WW2), ambapo nchi za Marekani, Canada na Uingereza zimekusanya majeshi na vifaa huko Uingereza.

Ni Juni 6, 1943 na nchi hizi washirika zimeamua rasmi kwenda kuikomboa nchi ya Ufaransa kwa kuanzia Normandy ambalo ni eneo la kimkakati, wakati huo Ujerumani ikiwa imejizatiti
kwa kujenga ngome imara na silaha kali sana.

Wana manowari za kivita zaidi ya 5,000, wana ndege vita zaidi ya 13,000 na wanajeshi zaidi ya 160,000 walio tayari kwa vita na sasa wanasubiri amri tu.

Hii ni baada ya ndege vita za Japan kuishambulia manowari ya Marekani mnamo Novemba 13, 1942 na kuizamisha na wanajeshi wengi wa nchi hiyo kupoteza maisha yao wakiwemo
wanandugu watano wa tumbo moja.

Wanandugu hao ambao ni watoto wa Thomas Sullivan ni Joe, Matt, Al, Frank na George na jozi zaidi ya 30 za wanandugu wengine. Jambo hili la kuwaweka ndani ya kikosi kimoja
vitani wanandugu halikuwa la kawaida ndani ya Jeshi la Marekani, na linalitikisa jeshi.

Kunaibuka simanzi kubwa baada ya tukio hili, simanzi inayolifanya jeshi kutunga kanuni za kuzuia wanandugu kuhudumu pamoja, kisha Bunge la Marekani likapitisha sheria inayoenda mbele zaidi ikitaka kama wanandugu watakuwa vitani, mfano wapo wawili na mmoja kufa itabidi aliyebaki arudishwe nyumbani ili kuepuka familia kupoteza watoto wote vitani.

Sasa baada ya sheria hii, ndani ya Jeshi la Marekani kuna wanandugu wanne wa familia ya Michael Niland wanaokwenda katika vita hii, wanandugu hawa ni Preston, Robert, Edward na Frederick (Fritz), ambaye kwenye filamu hii anajulikana kama James Ryan.

Hawa ni wanajeshi wakihudumu vikosi tofauti wakati wa vita hiyo. Inapofika mwishoni mwa Mei 1944, familia ya Michael Niland wanapokea taarifa ya kifo cha Edward kuwa ametunguliwa uko Burma na Wajapani na hajapatikana.

Juni 6, 1944 wanapokea taarifa nyingine kuwa Robert naye amekufa wakati wa ukombozi  wa eneo la kimkakati la Normandy wakati  wa operesheni maalumu, siku ya pili yake Robert naye anakufa katika eneo la Omaha Beach.

Kwa taarifa hizi inaonesha kwamba familia ya Michael Niland wamebakiwa na mtoto mmoja tu, Frederick (Fritz) Niland, ambaye kwenye filamu hii ndiye James Ryan, askari wa cheo cha Private na bahati mbaya jeshi halijui yuko wapi na kikosi gani.

Mkuu wa Wafanyakazi katika Jeshi la Marekani, Father Francis anaagiza kuwa Private James Ryan atafutwe haraka popote alipo na kwa gharama yoyote ile ili arudishwe nyumbani na familia isipoteze watoto wote.

Madhumuni ya kumtafuta ni ya kipropaganda zaidi kwani kurudi kwa Private Ryan kutaongeza morali nyumbani. Wanaambiwa kuwa mama yake, tayari ameshapoteza watoto
watatu vitani, na hatakiwi kumpoteza na huyu mmoja aliyebaki.

Kumbuka kuna sheria mpya na hivyo Private Ryan anapaswa kurudishwa nyumbani. Jukumu la kumtafuta Private Ryan anakabidhiwa Kapteni Miller na kikosi chake cha watu wanane.

Lakini wanajeshi hawa wanane wanaopewa kazi hii pia wana wazazi na zaidi,  amefundishwa kuua Wajerumani, si kuhatarisha maisha yao wakimtafuta mtu. “Huyu Private Ryan ana thamani yake,” mmoja wa wanajeshi hawa analalamika.

Sasa kazi ya kumtafuta Private Ryan inaanza, wanajeshi hawa wanamsaka kikosi kimoja hadi kingine na katika harakati hizo wanakumbana na tabu kubwa.

Kunatokea mauaji na hasara kubwa sana na haikuwa kazi rahisi kumpata Private Ryan, na hata wanapofanikiwa kumpata bado inakuwa kazi ngumu kumshawishi arudi nyumbani.

Hata hivyo, baadaye anarudishwa Marekani kupitia Uingereza baada ya kutokea maafa zaidi.

Inapofikia mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia inagundulika kuwa kaka wa Private Ryan, Edward aliyedhaniwa kuwa amekufa huko Burma yupo hai na anakombolewa na vikosi vya Uingereza kutoka mikononi mwa Wajapani na kisha kukabidhiwa Marekani, huku ndugu wengine wawili, Preston na Robert waliokufa wanazikwa jirani.

Si rahisi kuyaelezea yote yaliyotokea kwa mara moja lakini itapendeza ukiitafuta ukaona jinsi filamu hii inavyotoa somo kubwa ikionesha mambo kuhusu vita ambayo ni magumu
mno kuyaelezea.

Mwongozaji gwiji wa filamu za Hollywood, Steven Spielberg anajua jinsi ya kuwafanya watazamaji wake kusisimkwa na wakati mwingine kutokwa na machozi kuliko mwongozaji
yeyote tangu filamu ya Chaplin ya “City Lights.”

Hii ni filamu iliyotoka mwaka 1998 ikiwa imetengenezwa kutokana na visa vya kweli vilivyotokea wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, pale nchi washirika walipoamua kuikomboa Ulaya kwa kuanzia kuikomboa Ufaransa mnamo Juni 6, 1943.

Saving Private Ryan ni moja kati ya filamu bora kabisa za kivita, na inasemwa kuwa ndiyo filamu bora ya kivita ya wakati wote, ikiwa imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 70 na imefanikiwa kuingiza dola milioni 482.3 kupitia maonesho ya filamu.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

 

Related Articles

Back to top button