Mastaa

Ulevi wamponza Britney Spears

NEWYORK: MWANAMUZIKI maarufu wa Marekani Britney Spears amekamatwa na polisi katika Jimbo la California baada ya kuripotiwa kuendesha gari kwa hatari barabarani kwa takribani saa moja kabla ya kusimamishwa na kukamatwa kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, Spears mwenye umri wa miaka 44 alikamatwa majira ya saa 3:30 usiku wa juzi katika eneo la Ventura County baada ya kuonekana akiendesha gari lake aina ya BMW kwa kuyumba-yumba na kubadilisha njia mara kwa mara katika Barabara Kuu ya 101.

Rekodi ya mawasiliano ya dharura ya 911 iliyopatikana imeonesha askari na wahudumu wa kituo cha mawasiliano wakifuatilia gari hilo kwa karibu huku wakitoa taarifa za mwenendo wa dereva huyo.

Katika mawasiliano hayo, mmoja wa wahudumu amesema: “Kuna gari aina ya sedan jeusi, linapunguza mwendo ghafla, linayumba barabarani na linaonekana halina taa ya nyuma.”

Baadaye askari waliweza kulisimamisha gari hilo na kuanza kuzungumza na dereva kabla ya kuanza taratibu za uchunguzi.

Katika hatua ya awali, askari waliomba aitwe mtaalamu wa kutambua matumizi ya dawa za kulevya (Drug Recognition Expert) ili kufanya tathmini kama dereva alikuwa amelewa pombe au kutumia dawa nyingine.

Baada ya kukamatwa, Spears aliachiliwa kwa dhamana na anatarajiwa kufikishwa mahakamani Mei 4 mwaka huu kujibu tuhuma zinazomkabili.

Spears, ambaye aliwahi kutamba duniani kupitia nyimbo kama “Toxic”, amekuwa akipitia changamoto za maisha binafsi kwa miaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa familia uliosababisha kuwekwa chini ya uangalizi wa kisheria (conservatorship) kwa miaka 13 kabla ya kuondolewa mwaka 2021.

Related Articles

Back to top button