Burudani

Mr Blue aweka tiki kwa Marioo mbele ya Mbosso

DAR ES SALAAM: MKALI wa muziki wa hip hop nchini, Khery Sameer Rajab (Mr Blue), amesema wazi kuwa kati ya wasanii wawili wakubwa wa Bongo Fleva, Omary Mwanga (Marioo) na Mbosso Khan, angechagua kumsapoti Marioo akieleza kuwa ni msanii jasiri kwa kuthubutu kushindana na Mbosso.

Akizungumza katika mahojiano yake, Mr Blue amesema kuwa Mbosso ana uzoefu mkubwa zaidi kimuziki, jambo linalomfanya aonekane kama “kaka” katika tasnia hiyo, huku Marioo akionekana kama mdogo aliyethubutu kusimama imara dhidi ya mkongwe wake.

“Aaah! Mimi nikisema nichague mmoja, nitamchagua Marioo. Kwa sababu Mbosso na Marioo, Mbosso ni mkubwa kimuziki,” amesema Mr Blue.

“Historia ya Mbosso yamweka juu
Mr Blue amefafanua kuwa Mbosso amepitia safari ndefu katika muziki, akianza tangu enzi za awali alipokuwa akitambulika kwa jina la Marombosso, kabla ya kufika alipo sasa.

“Watu wengi hawajafuatilia, Mbosso alikuwa anaitwa Marombosso, ameshakuwaga kule (ya baridi) kitambo na akafanya mambo makubwa,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Mr Blue, uzoefu huo unampa Mbosso nafasi ya kuwa juu kimuziki, lakini kitendo cha Marioo kuweza kuwekwa katika ushindani wa moja kwa moja naye, tayari kinaonyesha ukubwa wake katika tasnia.

Marioo aonekana Jasiri
Mr Blue amesema kuwekwa kwa Marioo kushindana na Mbosso ni ishara tosha kwamba Marioo naye ni msanii mkubwa, mwenye uwezo na ujasiri wa hali ya juu.

“Kumuweka Marioo kushindana na Mbosso tayari Marioo kaonekana naye ni mkubwa,” amesema.

Mr Blue ametumia mfano wa kifamilia kueleza msimamo wake:
“Kimuziki Mbosso ni kaka wa Marioo. Kwa hiyo namchagua Marioo kwa sababu mmepeleka mtoto na kaka wakapigane, halafu uniambie nimshangilie nani? Mimi namshangilia dogo, kwa sababu ana uwezo wa kupigana na kaka — huo ni ujasiri mkubwa sana,” amesema Mr Blue.

Kauli hiyo imezua mjadala miongoni mwa wadau wa muziki na mashabiki wa Bongo Fleva, wakitafakari nafasi ya kila msanii na maana halisi ya ujasiri katika ushindani wa kisanaa.

Related Articles

Back to top button