Makonda awataka Watanzania kuunga mkono vipaji vya ndani

DAR ES SALAAM:WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kupenda na kuunga mkono vipaji vya ndani, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa shule na viwanja vya michezo kwa lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Makonda amesema maendeleo ya michezo nchini yanahitaji mshikamano wa kitaifa na imani kwa vipaji vilivyopo ndani ya nchi, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Makonda amempongeza Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed ‘Gamondi’ Morocco, kwa kazi nzuri aliyofanya, akieleza kuwa uamuzi wa kumbakiza ulitokana na uelewa wake mzuri wa wachezaji wa Kitanzania na uwezo wake wa kuwatumia kwa ufanisi.
“Tumepokea wasifu wa makocha wengi, lakini tukaona ni vyema kubaki na kocha anayewafahamu wachezaji wetu na anajua namna bora ya kuwatumia,” amesema Makonda.
Aidha, aliwataka wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchi kurejea nyumbani na kuisaidia Taifa Stars ili kuongeza ushindani na kuhakikisha timu inapata mafanikio makubwa katika mashindano ya Afrika.
Akizungumzia mashindano ya Ramadhan Cup, Makonda amesema hayakuanzishwa na Serikali bali ni juhudi za wadau wa dini, akibainisha kuwa muingiliano wa mwezi wa Ramadhan na kipindi cha Kwaresima ni jambo jema kiimani na linaloimarisha mshikamano wa kijamii.




