TFF yawataka Futsal kukamilisha kazi Ivory Coast

DAR ES SALAAM: KAIMU Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Mirambo, ameihimiza Timu ya Taifa ya wanaume ya Futsal kuhakikisha inalinda ushindi na kumaliza kazi vizuri katika mchezo wa pili wa kufuzu Futsal AFCON 2026 dhidi ya Ivory Coast.
Mirambo aliyasema hayo alipozungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi mara baada ya Tanzania kuibuka na ushindi wa mabao 7-3 katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ya kufuzu uliochezwa Uwanja wa New Amaan Zanzibar jana, akisisitiza kuwa lengo kubwa ni kufuzu kucheza fainali za AFCON.
“Tuhakikishe tunamaliza vizuri. Lengo letu ni kufuzu kwenda kucheza AFCON. Ukishinda mchezo wa kwanza halafu ukapoteza wa pili hutakumbukwa, hivyo ni muhimu kulinda ushindi huu,” alisema Mirambo.
Aliwapongeza wachezaji kwa ushindi mkubwa walioupata, huku akiwataka kuendelea kuwa na umakini na morali ya ushindani katika mchezo wa marudiano utakaochezwa ugenini.
“Hatuna muda mrefu wa maandalizi, kesho mtasafiri kwa ajili ya mchezo wa pili. Rudisheni kila nguvu, ile nguvu mliyoanza nayo iendelee hadi mwisho,” aliongeza.
Kwa upande wake, mchezaji wa Timu ya Taifa ya wanaume ya Futsal, Awadhi Juma, alisema ushindi walioupata umeongeza ari na imani kwa wachezaji, lakini akakiri kuwa bado wana kazi kubwa mbele yao.
Aliwaomba Watanzania kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa mchezo wa pili utachezwa ugenini.
Mwisho




