Modrić aondoka akiwa ameandika historia kubwa ya Croatia

TORONTO:KIUNGO wa Croatia, Luka Modrić, ameaga rasmi Kombe la Dunia baada ya safari yake ya miaka mingi kufikia mwisho.
Akiwa na umri wa miaka 40, Modrić ameondoka akiwa mmoja wa wachezaji walioandika historia kubwa zaidi kwenye mashindano hayo, baada ya kushiriki Kombe la Dunia mara tano akiwa na timu ya taifa ya Croatia.
Mafanikio yake makubwa yalikuja mwaka 2018 alipoipeleka Croatia hadi fainali ya Kombe la Dunia na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano. Mwaka 2022 aliiongoza tena Croatia kumaliza katika nafasi ya tatu.
Katika maisha yake ya kimataifa, Modrić ameichezea Croatia mechi 202 na kufunga mabao 21, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa wachezaji walioichezea timu zao za taifa mara nyingi zaidi katika historia ya soka.

Pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza mchezo wa hatua ya mtoano katika Kombe la Dunia.
Ingawa safari yake kwenye Kombe la Dunia imehitimishwa, mchango wa Luka Modrić kwa Croatia na soka la dunia utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo.




