Riyad Mahrez atangaza kustaafu kuichezea Algeria

BAADA ya safari ya Algeria kumalizika kwenye Kombe la Dunia, nahodha wa timu hiyo, Riyad Mahrez, ametangaza rasmi kustaafu kuichezea timu ya taifa.
Mahrez alitoa taarifa hiyo mara baada ya Algeria kuondolewa kwenye mashindano hayo, akithibitisha kuwa mechi hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kwake akiwa na jezi ya taifa lake.
“Hii ilikuwa mechi yangu ya mwisho kwa timu ya taifa,” amesema Mahrez katika mahojiano na beIN Sports.
Mahrez anamaliza safari yake ya kimataifa akiwa ameichezea Algeria mechi 119, akifunga mabao 40 na kutoa asisti 45. Pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa AFCON 2019, mafanikio yanayomuweka kwenye historia ya soka la nchi hiyo.
Mbali na mafanikio akiwa na timu ya taifa, Mahrez pia alitunukiwa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 2016, na kwa miaka mingi amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi kuwahi kuitumikia Algeria.
Kuondoka kwake kunafunga ukurasa wa mmoja wa mastaa wakubwa katika historia ya soka la Algeria, huku akiacha urithi mkubwa ambao utadumu kwa miaka mingi.




