Dube anaitamani Yanga hadi basi

MSHAMBULIAJI wa Kimataifa kutoka Zimbabwe Prince Dube ameonyesha kuipenda timu anayodaiwa kujiunga nayo kwa msimu ujao wa 2024/25 baada ya kuweka picha inayomuonyesha akiwa na furaha mno wakati akimpongeza Rais wa Klabu ya Yanga Injinia Hersi Said kwa kumshika kichwa huku akiandika “huwezi kuficha furaha yako sehemu yenye furaha”
Mchezaji huyo aliyeikacha Azam FC ya Chamazi kwa sababu zake binafsi anazungumzwa kujiunga na miamba ya Jangwani Yanga SC timu ambayo inatajwa anaipenda mno huku akiamini ndiyo itakayomuwezesha kunyanyua vikombe kwa msimu ujao.
Dube aliweka ujumbe huo na picha hiyo katika ukurasa wake wa facebook na katika mchezo wa jana wa ‘Wape Tabasamu’ ambao ni mchezo wa hisani uliokuwa na lengo la kuchangia asilimia 30 ya mapato yote ya getini kwenye sekta ya afya.
Dube a na Injinia Hersi walikuwa timu Dickson Job iliyoshinda mabao 6-2 huku wachezaji hao wawili wakifunga bao moja moja kila mmoja.
Tukio lililosababisha picha hiyo kupigwa ni baada ya Injinia Hersi kufunga goli la kwanza kwa kupiga kichwa safi akiunganisha krosi ya Denisi Nkane ambapo goli hilo liliibua shangwe na wachezaji takribani wote wa timu Job walimkimbilia injinia Hersi na kumlaki kwa namna zao.
Dube alikiwa miongoni mwao alianza kwa kuruka juu ya wachezaji wengine lakini baada ya hapo alimfuata tena Hersi na kumshika kichwa akimpongeza huku akionekana kujawa na furaha mno baada ya bao hilo.
Wengi walioiona picha hiyo wameeleza maoni yao kwamba hakuna shaka mchezaji huyo atatua Jangwani kukipiga pamoja na wachezaji mahiri akiwemo Pacome na Aziz Ki.
Dube hajaonekana muda mrefu kushiriki katika mechi za kuonekana na watu wengi kama alivyokuwa Azam FC lakini namna alivyocheza mchezo wa jana na kufunga kwa kichwa safi akimjibu injinia Hersi ameonekana kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki waliokuwepo katika uwanja huo wa Jamhuri mkoani hapa.
Licha ya Dube kuhusishwa kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na miamba hiyo ya Jangwani mchezaji mwingine anayedaiwa kumalizana na Yanga kwa mkataba wa awali wa miaka miwili ni beki wa kushoto Chadrack Boka kutoka Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).