
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam leo imemtambulisha raia wa Zambia, Andre Mtine kuwa Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa timu hiyo.
Mtine anachukua nafasi ya Senzo Mazingiza aliyeachia ngazi Julai 31, 2022 baada ya mkataba wake kwisha.
“Ni heshima kubwa kuwa Mtendaji mkuu wa Yanga, najua Yanga Sc ina historia kubwa ndio maana nimechagua kufanya kazi hapa, natambua nafasi kubwa ya wale wote ambao wamefanya kazi kubwa kufikisha Yanga hapa ilipo”
amesema Mtendaji mkuu wa Yanga, Andre Mtine.
Awali Rais wa Yanga, Hersi Said amesema uchaguzi wa mtendaji huyo mpya ulipita katika mchakato wenye uadilifu mkubwa.

“Tunafahamu katika mfumo wa sasa CEO ndiye mtendaji mkuu wa klabu yetu, wiki kadhaa tulitangaza nafasi hiyo na tuliteua kamati ndogo ya kupitia maombi hayo na leo kwa heshima kubwa tunamtangaza CEO wa Klabu yetu Bwana Andre Mtine” Amesema Rais wa Yanga Eng. Hersi Said.
Kabla ya kujiunga na Yanga Mtine alifanya kazi katika klabu za Buildcon, Nkana, Zesco, Shirikisho la soka la Zambia na klabu ya TP Mazembe ya Jamhauri ya kidemokeasi ya Congo-DRC ambayo amekuwa Mtendaji ndani ya Klabu hiyo kwa miaka 12.