Copco yaipania Yanga

DAR ES SALAAM: TIMU ya First League (Daraja la Pili) ya Copco imesema itautumia mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga kuonesha ubora wa wachezaji wake.
Copco itakutana na Yanga Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam kusaka ushindi utakaowawezesha kusonga mbele hatua inayofuata.
Meneja wa timu hiyo Juma Kisuse ameliambia Spotileo kuwa inakwenda kucheza na timu kubwa hivyo, ni nafasi kwa wachezaji wake kuonesha vipaji vyao na ubora kujiweka sokoni.
“Tunaamini Yanga ni timu kubwa na kila mtu anatamani kucheza nao. Ni mchezo ambao wachezaji wetu wanahitaji kujiuza na kupata soko zaidi,”amesema.
Timu hiyo inatarajiwa kufika Dar es Salaam leo ili kufanya maandalizi ya mwisho ya kujiandaa na mchezo huo.
Copco iliyoko kundi B First League inashika nafasi ya sita kwa pointi tano ilizovuna katika michezo saba.