Zari: Kujitegemea hakumaanishi kutokuolewa

MSANII na mfanyabiashara Zari Hassan ‘Zari The Boss Lady’, ambaye ni mzazi mwenza wa mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, amefafanua kauli yake ya kuwataka wanawake kuwa huru kiuchumi, akisema hakumaanisha kuwa wanawake wasiolewe au wasiwaheshimu waume zao.
Zari amesema kauli hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti, huku baadhi ya watu wakimuelewa na wengine kuichukulia tofauti na alivyokusudia.
Akizungumzia suala hilo, Zari amesema alipowahimiza wanawake kujenga uwezo wa kifedha, lengo lake lilikuwa kuwashauri wawe na uwezo wa kujitegemea na kufanya maamuzi yao bila kutegemea kabisa mtu mwingine.
“Ninapowaambia wanawake waamke na wawe na uhuru wa kifedha, simaanishi kwamba msiolewe.
Simaanishi kwamba msimheshimu mwanaume wenu. Mimi namheshimu mume wangu,” amesema Zari.
Amesema amefanya kazi ya kujijenga kiuchumi na anaamini mwanamke anaweza kuwa na mafanikio yake huku akiwa katika ndoa na akimheshimu mwenza wake.
“Mimi nimejijenga vizuri sana na ninajitegemea kabisa kifedha,” amesema.
Zari pia amezungumzia safari yake ya maisha, akisisitiza kuwa amekuwa akijijenga na
kujitambulisha kama mwanamke mwenye mafanikio tangu miaka ya nyuma, kabla ya umaarufu wake kufikia kiwango alichonacho sasa.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakimfahamu kutokana na maisha yake ya sasa, bila kufahamu safari aliyopitia kabla ya kufikia mafanikio hayo.
Kwa upande mwingine, Zari amesisitiza kuwa ujumbe wake kwa wanawake ni umuhimu wa kujenga uwezo wao kiuchumi, huku akitambua kuwa kila mwanamke anaweza kuwa na mtazamo wake kuhusu ndoa na mahusiano.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mjadala kuhusu wanawake kujitegemea kiuchumi na nafasi yao katika familia ukiendelea kupata tafsiri tofauti katika jamii, hasa kupitia mitandao ya kijamii.




