Muziki

AliLIKiba: ‘Hadithi’ Ndio wimbo wangu wenye ubunifu mkubwa

MSANII nyota wa muziki wa Bongo Fleva nchini, Ali Kiba ‘King Kiba’, amesema kuwa kati ya nyimbo zote alizowahi kuzitunga na kuzirekodi katika safari yake ya muziki, wimbo wa Hadithi ndio alioutengeneza kwa ubunifu wa hali ya juu zaidi.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo wimbo huo wa zamani umeanza kupata umaarufu mpya katika mtandao wa TikTok, huku mashabiki wengi wakitumia sehemu mbalimbali za wimbo huo kutengeneza video na maudhui yanayovutia.

Akizungumzia mafanikio hayo mapya, Alikiba amesema muziki una siri nyingi ambazo wakati mwingine huufanya wimbo kuendelea kuishi na kupendwa hata baada ya miaka mingi tangu kutolewa kwake.

“Muziki una siri. Nadhani Hadithi ni moja ya classic songs nilizowahi kufanya kwa ubunifu mkubwa sana,” amesema Alikiba.

Msanii huyo ameeleza kuwa wakati wa kuutengeneza wimbo huo alitumia uwezo mkubwa wa kiuandishi na ubunifu wa kipekee katika kuwasilisha ujumbe wake, jambo ambalo linaendelea kuwavutia wasikilizaji hadi sasa.

Kurejea kwa kasi kwa wimbo wa Hadithi kwenye TikTok kumedhihirisha namna kazi bora za muziki zinavyoweza kuvuka muda na kuendelea kugusa hisia za mashabiki wa vizazi tofauti.

Mashabiki wengi wa Alikiba wamekuwa wakitoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii wakieleza kuwa Hadithi ni miongoni mwa nyimbo bora zilizowahi kutolewa na msanii huyo, huku wengine wakisifu ubora wa mashairi, ujumbe na mtindo wake wa kipekee.

Mafanikio hayo yanaendelea kuthibitisha nafasi ya Alikiba kama mmoja wa wasanii wenye mchango mkubwa katika historia ya muziki wa Tanzania, akiwa na uwezo wa kutengeneza nyimbo zinazobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki kwa muda mrefu.

Related Articles

Back to top button