Muziki

Paula Clement kuongoza Super Sunday Mabibo External

DAR ES SALAAM: MSANII wa nyimbo za Injili nchini, Paula Clement, anatarajiwa kupamba Tamasha la Super Sunday litakalofanyika Agosti 23, 2026 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mabibo External, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Spoti LEO, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa KKKT Mabibo External, Erick Kisaule, amesema tamasha hilo la kusifu na kuabudu litawakutanisha waimbaji mbalimbali, wakiwemo kwaya za usharika pamoja na Paula Clement.

Kisaule amesema lengo la tamasha hilo ni kuwakutanisha vijana, kuimarisha afya zao kupitia kusifu na kumwabudu Mungu, huku wakiwezeshwa kujenga maadili mema kupitia burudani na mafundisho ya kiroho.

Amesema tamasha hilo ni sehemu ya juhudi za kanisa kuwashirikisha vijana katika shughuli zenye manufaa kwa maendeleo yao ya kimwili, kiakili na kiroho, pamoja na kuwajenga katika mshikamano na urafiki.

“Matamasha ya aina hii yanawasaidia vijana kujumuika pamoja, kujenga urafiki na kuachana na tabia zisizofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na mienendo mingine inayoweza kuathiri mustakabali wao,” amesema Kisaule.

Kwa mujibu wa Kisaule, tamasha hilo litaanza saa sita mchana hadi jioni na litakuwa wazi kwa vijana wote bila kujali madhehebu yao.

Ameongeza kuwa mbali na burudani, washiriki watapata ujumbe wa kiroho wenye lengo la kuwajenga vijana katika maadili mema na kuwasaidia kumkaribia Mungu zaidi.

Amesema neno litakaloongoza tamasha hilo linatokana na maandiko yanayosema: “Jinsi gani kijana ajisafishe njia yake? Kwa kutii na kulifuata neno la Mungu.”

Kisaule amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo, akieleza kuwa halitakuwa na kiingilio na litatoa nafasi kwa vijana kujumuika, kusifu, kujifunza na kuburudika kwa pamoja.

“Tunawakaribisha vijana wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hili muhimu la kujenga afya, umoja na maadili. Hakuna kiingilio; ni bure kula, kunywa na kucheza,” amesema Kisaule.

Related Articles

Back to top button