BASATA yapanga mageuzi sekta ya sanaa na uchumi wa ubunifu

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeweka mkakati wa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya sanaa na uchumi wa ubunifu nchini kwa kuboresha mazingira ya kazi za wasanii, ikiwemo upatikanaji wa hakimiliki, leseni na masoko ya bidhaa za ubunifu.
Akizungumza katika Maonesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026, Afisa Sanaa Mwandamizi wa BASATA, Augustino Mkame, kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, amesema baraza hilo linaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wasanii na wadau wa sanaa kunufaika zaidi na kazi zao.
Mkame amesema BASATA imejikita katika kutoa elimu, ushauri na miongozo kwa wasanii ili kuongeza ubora wa kazi zao na kuhakikisha zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Lengo letu ni kuona wasanii wanapata mazingira bora ya kufanya kazi, wanatambua haki zao za msingi na kunufaika na fursa zinazopatikana kupitia sekta ya sanaa na ubunifu,” amesema Mkame.
Ameeleza kuwa BASATA inaunga mkono majukwaa mbalimbali ya ubunifu yanayowawezesha wasanii kukutana, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya, kukuza vipaji pamoja na kupata fursa za kutangaza na kusambaza kazi zao katika masoko tofauti.
Kwa mujibu wa Mkame, majukwaa hayo yana mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa ubunifu unaotoa ajira, kuongeza kipato kwa wasanii na kuimarisha mchango wa sekta ya sanaa katika maendeleo ya taifa.
Aidha, amewahimiza wasanii na wadau wa sanaa kushiriki kikamilifu katika maonesho na majukwaa ya ubunifu yanayoandaliwa ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa ushirikiano ni nyenzo muhimu ya kukuza ushindani wa kazi za wasanii wa Afrika Mashariki katika soko la kimataifa.
“Kadiri tunavyoshirikiana na kuunganisha nguvu, ndivyo tunavyoweza kujenga sekta imara ya sanaa na ubunifu yenye uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesisitiza.
Maonesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026 yanafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 18 hadi 21, 2026, yakikusanya wadau mbalimbali wa sanaa, ubunifu na biashara kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kuhamasisha ukuaji wa uchumi wa ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki.




