Mwalimu aongeza joto, Simba, Yanga zikicheza leo

ZANZIBAR: KABLA ya filimbi ya kwanza ya mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba, usiku wa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Seleman Mwalimu tayari ameongeza joto la pambano hilo baada ya kuhamia Yanga akitokea Simba siku chache kabla ya mchezo.
Mwalimu, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba hadi hivi karibuni, sasa anaweza kukutana na waajiri wake wa zamani akiwa amevaa jezi ya Yanga, jambo lililoongeza mjadala miongoni mwa mashabiki wa timu hizo.
Hata hivyo, makocha wa pande zote mbili, Steven Barker wa Simba na Manqoba Mngqithi wa Yanga, wamejaribu kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo wenyewe, huku kila mmoja akiahidi ushindani mkubwa.
Barker amesema Simba imejiandaa vizuri na inaingia uwanjani kwa lengo la kutwaa taji hilo na kuanza msimu kwa mafanikio.
Kwa upande wake, Mngqithi amesema Yanga imejiandaa vizuri licha ya muda mfupi wa maandalizi, na kwamba haitatazama ushindi pekee, bali pia itataka kuonesha soka litakalowafurahisha mashabiki wake.
Timu zote mbili zimetoka kupoteza katika matamasha yao, Simba ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi ya Kenya na Yanga ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Aigles du Congo.
Rekodi
Simba inaongoza kwa kutwaa mataji mengi ya Ngao ya jamii mara 10, kuanzia rasmi mwaka 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019,2020 na 2023.
Kwa upande wa watani zao wa jadi Yanga inafuatia kwa kuchukua ubingwa huo mara tisa tu, ikianza mwaka 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022, 2024 na 2025, huku Azam, ikichukua mara moja mwaka 2016, sawa na Mtibwa Sugar iliyolichukua 2009.
Mwamuzi mwenye beji ya FIFA, Ahmed Arajiga atasimamia mchezo huo, atasaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga, Leonard Mkumbo wa Manyara huku wa akiba akiwa Nassir Siyah wa Zanzibar. Mechi kamishna wa mchezo huo atakuwa Soud Abdi wa Arusha.
Taarifa iliyotolewa na TFF ni kwamba waamuzi hao wote watasaidiwa na teknolojia maalum ya Football Video Support (FVS), kuwasaidia kuamua matukio ya utata kwenye mchezo huo.




