Aweso awataka coastal union kuifanya mkwakwani ngome

TANGA: WAZIRI wa Maji, Juma Aweso, amewataka mashabiki wa Coastal Union kuendelea kuishika mkono timu hiyo huku akiwataka viongozi wa klabu kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana ili kuipa Tanga mafanikio katika msimu mpya.
Aweso amesema hayo jana wakati wa tamasha la Coastal Union, akisisitiza kuwa mashabiki na wakazi wa Tanga wanataka kuona timu yao ikifanya vizuri, hasa katika michezo ya nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
“Mkataa kwao ni mtumwa. Mashabiki wa Coastal Union tuendelee kuishika mkono timu yetu, tuhakikishe inafanya vizuri. Lakini kubwa, tuwape deni viongozi wetu wa Coastal, mashabiki na Watanga wanataka ushindi katika uwanja wetu wa nyumbani,” amesema Aweso.
Amesema matarajio ya mashabiki ni kuona Coastal Union ikifanya Uwanja wa Mkwakwani kuwa ngome ambayo timu pinzani zitapata wakati mgumu kupata matokeo, akiamini hilo linawezekana iwapo wadau wote wataendelea kuisapoti timu.
Aweso pia alitoa matumaini kwa mashabiki kwamba msimu huu Tanga inaweza kuwa miongoni mwa mikoa itakayosherehekea ubingwa, akisema ni jambo linalowezekana iwapo timu itaungwa mkono kwa nguvu.
Katika tamasha hilo lililolenga kuitambulisha Coastal Union kwa mashabiki wake kuelekea msimu mpya, timu hiyo ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Bandari FC katika mchezo wa kirafiki.
Matokeo hayo yameacha kazi kwa benchi la ufundi na wachezaji kuhakikisha wanafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kuanza kwa msimu mpya, huku mashabiki wakitarajia kuona Coastal Union ikiwa na ushindani mkubwa.




