Ligi KuuNyumbani

Makocha Yanga, Simba wafikiria ushindi

TAMBO, mikwara, majigambo, ngebe, majivuno na kila aina ushindani wa maneno vinatarajiwa kwisha jioni ya Oktoba 23 wakati watani wa jadi Yanga na Simba zitakapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Wakizungumza na Spotileo kwa nyakati tofauti makocha Juma Mgunda wa Simba na Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze wameelezea jinsi timu zao zilivyojiandaa kwa ajili ya mchezo huo katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema kila kitu kinakwenda sawa na wana kila sababu ya kushinda mchezo huo kutokana na maandalizi waliyofanya.

Amesema mchezo huo hautakuwa rahisi kwa timu zote mbili lakini anakipa kikosi chake nafasi kubwa ya kuondoka na pointi tatu baada ya wachezaji wake kumuonesha utayari wa kupambana.

“Ni mchezo wangu wa kwanza kuiongoza Simba katika mechi za Simba na Yanga, siyo mchezo rahisi hata kidogo lakini kama kocha kiongozi ningependa kuwa na mwanzo mzuri sababu kama nitapoteza basi hata yale mazuri niliyofanya kabla yatapungua thamani,” amesema Mgunda.

Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amejigamba kuwa mpaka kufika saa 1 kasoro jioni Oktoba 23 heshima ya Yanga itakuwa juu kuliko timu yoyote Tanzania.

Amesema mchezo huo dhidi Simba utatumika kama maandalizi kwa ajili ya mchezo wa mtoano wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

“Sisi tumepokea maneno yote ya kejeli lakini tutawajibu kwa vitendo Jumapili na kuonesha ukubwa wa Yanga, pamoja na kutolewa kwenye ligi ya mabingwa lakini bado timu ya Yanga ndio kubwa na bora kwenye soka la Tanzania,” amesema Kaze.

Amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na kinachofanyika hivi sasa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji.

Kaze pia ameahidi Yanga kuwatumia Bernard Morrison na Salum Abubakary ‘Sure Boy’ katika mchezo dhidi ya Simba.

“Hatuwezi kuongea mbinu zote ambazo tumepanga kuzitumia lakini wachezaji hao wawili ni sehemu ya kikosi kitakachocheza kesho dhidi ya Simba,” amesema Kaze.

Kocha huyo amesema kwa namna walivyoipania mechi hiyo matokeo mazuri kwao ni ushindi na wakitoka sare itakuwa ni sawa na kufungwa.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button