Kikapu

Stephen Curry ataka kustaafu Warriors

SAN FRANCISCO: HATMA ya nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry, imeingia sura mpya baada ya meneja mkuu wa klabu hiyo, Mike Dunleavy, kusema mchezaji huyo amepewa uhuru wa kuamua mwenyewe anataka kumalizia wapi maisha yake ya NBA, lakini bado anaamini ataendelea kuwa Warrior hadi anastaafu.

Curry, ambaye ameitumikia Warriors kwa miaka yote 17 ya maisha yake ya NBA, anaingia msimu wa mwisho wa mkataba wake unaomlipa dola milioni 62.5, jambo linalofungua uwezekano wa klabu hiyo na mchezaji kuanza mazungumzo ya mkataba mpya baada ya Agosti 29, 2026.

Dunleavy amesema hakuna dalili zinazoonesha Curry anataka kuondoka Golden State, akisisitiza kuwa ujumbe wa mchezaji huyo kwa muda mrefu umekuwa ni kutaka kumalizia kazi yake akiwa na Warriors.

“Anataka sana kushinda na anataka kumalizia maisha yake ya soka akiwa Warrior,” Dunleavy amesema, akieleza kuwa msimamo huo hauonekani kubadilika hata kama mkataba wake wa sasa unamalizika.

Hata hivyo, Warriors haijaweka pingu kwa Curry. Dunleavy amesema iwapo mchezaji huyo ataomba kuondoka, yeye pamoja na mmiliki wa klabu, Joe Lacob, watakaa chini na kulijadili suala hilo, kwa sababu Curry amefanya vya kutosha na anastahili kuamua hatma yake.

Curry, mwenye umri wa miaka 38, ameshinda mataji manne ya NBA akiwa na Warriors na mara mbili ametwaa tuzo ya mchezaji bora . Pia, amechaguliwa mara 11 kwenye kikosi cha All-NBA.

Lakini msimu uliopita ulikuwa mgumu kwake kutokana na majeraha, ambapo alianza michezo 41 pekee baada ya misimu miwili mfululizo akicheza angalau michezo 70.

Pamoja na changamoto hizo, Curry amewahi kusema angependa kucheza angalau misimu miwili zaidi kabla ya kustaafu, huku Warriors ikijaribu kujenga kikosi kitakachomsaidia kuwania ubingwa mwingine.

Warriors walimaliza msimu uliopita kwa rekodi ya ushindi 37 na kupoteza michezo 45, hali inayoweka presha zaidi kwa klabu hiyo kuimarisha kikosi ikiwa kweli inataka kumpa Curry nafasi ya kumalizia safari yake kwa mafanikio.

Related Articles

Back to top button