Masumbwi

Willilo aanza majukumu Afrika

ABUJA: RAIS wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lukelo Willilo, ameanza rasmi kutekeleza majukumu yake mapya ya Kaimu Katibu Mkuu wa African Boxing, chombo kinachosimamia mchezo wa ngumi za mtindo wa Olimpiki barani Afrika.

Willilo alianza kutekeleza majukumu hayo Novemba 9, mwaka huu, baada ya kuteuliwa na Rais wa African Boxing, Solomon Kargbo, na kuthibitishwa na Bodi ya Wakurugenzi katika kikao kilichofanyika Novemba 2, 2026.

Uteuzi huo unampa Willilo nafasi muhimu katika uongozi wa ngumi barani Afrika, huku Tanzania ikipata uwakilishi wa juu zaidi katika chombo hicho kinachosimamia na kuendeleza mchezo huo.

Mbali na nafasi hiyo mpya, Willilo pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya African Boxing na Mwenyekiti wa Kamati ya Mchezo na Mashindano ya shirikisho hilo.

African Boxing ni chombo kinachosimamia na kuendeleza ngumi za mtindo wa Olimpiki barani Afrika na ni mshirika wa World Boxing.

Uteuzi wa Willilo unatajwa kuwa fursa muhimu kwa Tanzania katika kushiriki kwenye maamuzi na mipango ya maendeleo ya ngumi za Olimpiki barani Afrika, ikiwemo masuala ya mashindano na uimarishaji wa mchezo huo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button