Fadhili Majiha amwendea ‘Msauzi’ Malawi

DAR ES SALAAM: BONDIA wa Ngumi za kulipwa nchini, Fadhili Majiha, mwenye nyota tatu na nusu kwa ubora Afrika ameweka wazi sababu ya kwenda nchini Malawi kuweka kambi kujiandaa na pambano lake dhidi ya Sabelo Ngebinyana kutoka Afrika Kusini.
Majiha anatarajia kupanda uliongoni Julia 20, 2024, mkoani Mbeya kutetea mkanda wa ubingwa wa Afrika pambano la raundi 10 la uzito wa kati, la WBC mkanda alioupata Oktaba 28, mwaka jana baada ya kumchapa Bongani Mahlangu kutoka Afrika Kusini.
Bondia huyo ameiambia Spotileo kuwa anatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Malawi kwa ajili ya kuweka kambi na kupata mbinu mpya kutoka kwa makocha wengine wa nchini humo katika gym ambayo ataenda kufanya maandalizi ya pambano hilo.
Amesema amemfatilia mpinzani wake huyo na ametumia Malawi kuwa ni nchi ambayo ataenda kupata maandalizi hayo na kuja kuendelea kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kutetea mkanda huo.
“Lazima nitoke niende nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ninaimani kubwa ya kwenda kupata mbinu na ujuzi kutoka kwa makocha wengine kutoka kambi nitakayoenda kufanya mazoezi, nimemtazama mpinzani wangu, ninaimani nitafanya vziuri.
Nahitaji kushinda hili pambano kwa sababu nikipigwa na Sabelo nitapoteza mkanda ambao natakiwa kuutetea mara mbili baada ya pambani hili la Mbeya na kushinda, natakiwa kucheza mechi ya mwisho kwa ajili ya mkanda wa WBC kuwa wangu kabisa,” amesema Majiha.