Ligi Kuu

Janza avutiwa na miundombinu Bunju

DAR ES SALAAM: MKURUGENZI mpya wa Ufundi wa Simba, raia wa Zambia, Honour Janza, amepongeza miundombinu ya klabu hiyo iliyopo Bunju Mo Arena, akisema ni ndoto ya kila klabu kuwa na mazingira bora ya kuendeleza soka.

Janza, ambaye alitambulishwa hivi karibuni katika nafasi hiyo, amesema amevutiwa na mazingira ya klabu hiyo pamoja na kiwango cha wachezaji anaowakuta katika mazoezi, akieleza kuwa anaamini Simba ina nafasi kubwa ya kuendelea kupiga hatua kutokana na historia na uwekezaji wake.

Akizungumza baada ya kuwatembelea wachezaji kwenye mazoezi yaliyofanyika katika Uwanja huo, Janza amesema ni fursa kubwa kwake kufanya kazi ndani ya klabu yenye historia na mafanikio makubwa barani Afrika na Tanzania, huku akiahidi kushiriki katika juhudi za kuendeleza soka.

“Ninaamini Simba ni klabu yenye historia kubwa barani Afrika na hata hapa Tanzania. Hii ni fursa ya kuchangia maendeleo ya kweli ya soka na kuendeleza historia ya klabu hii. Namshukuru Mungu kwa nafasi hii,” amesema.

Amesema alipofika Bunju Mo Arena na kuona miundombinu iliyopo, alitambua kuwa ni mazingira ambayo kila klabu na mwanamichezo anatamani kuwa nayo, akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni msingi muhimu katika maendeleo ya mchezo.

Janza amesema baada ya kukutana na benchi la ufundi, kocha na wachezaji, amevutiwa na namna kikosi kinavyojiandaa, akieleza kuwa kiwango cha wachezaji kinaonesha taaluma na umakini katika mazoezi.

Amesema kwa kuangalia mazoezi ya wachezaji, anaweza kubaini kuwa kila mmoja ana uwezo binafsi na anaonesha sifa za mchezaji wa kulipwa, jambo linalompa matumaini katika kazi yake mpya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button