Mabondia 79 kuchuana Klabu bingwa taifa

TANGA: MABONDIA 79 kutoka katika klabu 15 nchini wameanza kuchuana katika mashindano ya klabu bingwa taifa 2026, yanayotarajiwa kumalizika Agosti 30, katika viwanja vya Mkwakwani, Tanga.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na kutoa fursa kwa mabondia kuonesha uwezo wao, huku yakilenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya mchezo wa ngumi nchini.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo, klabu zilizoshiriki ni Ngome, MMJKT, Magereza, Tanga, Band Coy, Jenerali Chande, Mgulani JKT, Mashujaa, Makolola, Jeba, Black Eagle, Mkinga, Handeni, Magereza Chuo na Milongo MZA.
Amesema mbali na kuwania ubingwa wa taifa, mashindano hayo yatatumika pia kutathmini na kuchagua mabondia wenye uwezo wa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
Willilo amesema mabondia watakaoonesha kiwango bora, pamoja na washindi wa mashindano, watazingatiwa kwa ajili ya kuitwa kwenye kikosi cha Taifa kitakachojiandaa kushiriki mashindano ya ubingwa wa Afrika yatakayofanyika DRC mwezi Oktoba 2026.
“Shirikisho la Ngumi Tanzania linawaalika wananchi wa Tanga, mashabiki wa ngumi na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Mkwakwani kushuhudia ushindani wa mabondia kutoka klabu mbalimbali nchini,”amesema.




