Job: Kila mchezaji anapambana kupata namba Yanga

ZANZIBAR: BEKI wa Yanga, Dickson Job, amesema kambi ya timu hiyo inayoendelea Zanzibar imekuwa na ushindani mkubwa kwa wachezaji, kila mmoja akijitahidi kuonesha uwezo wake ili kumshawishi Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.
Job amesema uwepo wa kocha mpya umeongeza ari ya wachezaji kupambana na kuonesha viwango vyao, huku kila mmoja akitambua umuhimu wa kutumia vizuri nafasi alizonazo katika maandalizi ya michezo ijayo.
Akizungumzia hali ya kambi hiyo, Job alisema: “Kambi ni nzuri sana, kila mchezaji anapata ari ya kupambana ili kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Unajua mwalimu ni mpya, kwa hiyo kila mtu anajaribu kuonesha uwezo na kiwango chake. Kwa kweli kambi ni nzuri na tunaifurahia.”
Ameongeza kuwa ushindani uliopo kambini ni sehemu muhimu ya maandalizi ya timu hiyo, akisisitiza kuwa kila mchezaji ana wajibu wa kuonesha kiwango chake ili kumsaidia kocha kufanya maamuzi sahihi katika kupanga kikosi.
“Kila mchezaji lazima aoneshe kiwango chake ili mwalimu aweze kupata chaguo sahihi kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya kimataifa. Ni jukumu letu kama wachezaji kuonesha kile tulichonacho,” amesema Job.
Yanga ipo Zanzibar ikiendelea na maandalizi ya kujiweka tayari kwa michezo mbalimbali inayosubiri mbele yake, ikiwemo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo inahitaji maandalizi ya kutosha ili timu iweze kufanya vizuri.
Kambi hiyo inaongozwa na Kocha Mkuu Fadlu Davids, aliyejiunga na Yanga hivi karibuni akipewa jukumu la kuiongoza timu hiyo katika safari ya kuwania mafanikio kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.




