Wema Sepetu azindua kampeni ya kitaifa ‘

DAR ES SALAAM: Mwigizaji nyota nchini Tanzania, Wema Sepetu, ametangaza kuanzisha kampeni ya kitaifa iitwayo ‘Wema wa Mama’, inayolenga kuonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kupitia kampeni hiyo, Wema ataendesha makala maalum zenye ushahidi wa picha katika kila hatua, ambapo watazamaji watapata nafasi ya kusikia moja kwa moja kutoka kwa wananchi walioguswa na kunufaika na miradi mbalimbali ya serikali.
Aidha, katika kampeni hiyo, Wema atatembelea na kujionea miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za maji, afya, na elimu.
Lengo ni kuelewa kwa kina jinsi fursa za maendeleo zinavyotengenezwa na namna zinavyohitaji nguvu kazi, uwekezaji, pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi.
Kampeni ya Wema wa Mama inaadhimisha juhudi na mafanikio ya serikali katika maeneo ya kipaumbele kama miundombinu, afya, elimu, na kilimo, huku ikilenga kuhamasisha, kuunganisha na kuongeza ari ya maendeleo katika jamii nzima ya Watanzania.