Burudani

Wasanii wekezeni kwenye mirahaba mjenge utajiri’

DAR ES SALAAM: ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Victor Tesha, amewataka wasanii nchini kuwekeza mapato yanayotokana na kazi zao za ubunifu ili kujenga mali na kuhakikisha wanakuwa na kipato cha uhakika hata wanapostaafu au kushindwa kuendelea na shughuli za sanaa.

Amesema wasanii hawapaswi kutegemea mirahaba pekee, bali wanapaswa kutumia fursa za uwekezaji na huduma za kifedha zilizopo katika taasisi mbalimbali ili kukuza mapato yao na kujenga ustawi wa familia zao kwa muda mrefu.

Akizungumza Dar es Salaam leo katika hafla ya ugawaji wa tozo za hakimiliki kwa wasanii, Tesha amesema: “hatua ya sasa ya kugawa mirahaba ya zaidi ya Sh bilioni 1.3 ni matokeo ya safari ya muda mrefu ya kutetea haki na ustawi wa kiuchumi wa wabunifu nchini,”.

Amesema katika kipindi cha mwanzo cha Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Samia Suluhu Hassan aliteua kamati maalumu iliyokuwa na jukumu la kupitia maboresho ya sheria ili kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao, ambapo yeye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.

Akitoa pendekezo la kuongeza mapato ya wasanii, amesema taasisi zinazokusanya mirahaba zinapaswa kuangalia uwezekano wa kuwekeza sehemu ya fedha hizo katika mifumo salama ya uwekezaji kabla ya kugawa mapato kwa wenye haki.

Ametaja uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji ya pamoja, amana za muda maalumu katika benki na hati fungani za Serikali kuwa miongoni mwa njia zinazoweza kuchunguzwa ili fedha zinazokusanywa ziweze kuongezeka na kutoa manufaa zaidi kwa wasanii.

Amewashauri wasanii kutumia wataalamu wa fedha kutoka taasisi kama UTT, NBC, NMB na mifuko ya hifadhi ya jamii kupata elimu ya uwekezaji, bima na mipango ya kifedha badala ya kutegemea kipato kinachotokana na umaarufu pekee.

Amesema vipaji vya muziki, uandishi, uchongaji, uchoraji na ubunifu wa mifumo ya kompyuta vinaweza kuwa chanzo cha utajiri endapo vitasimamiwa vizuri na kuunganishwa na uwekezaji katika maeneo mengine ya uchumi.

Amewataka pia wasanii kutumia nafasi yao katika jamii kutoa taarifa sahihi kuhusu shughuli na fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali ili wananchi waweze kuzifahamu na kuzitumia.

Akizungumzia changamoto za teknolojia, amesema maendeleo ya akili unde (AI) yanaanza kuleta mabadiliko katika sekta ya ubunifu, hivyo wasanii wanapaswa kujiandaa kwa mazingira mapya ya ushindani na kutafuta njia nyingine za kuimarisha kipato chao.

Related Articles

Back to top button