Mapya yaibuka sakata la ‘P Diddy’
MSANII wa Muziki wa Hip Hop kutoka nchini Marekani Sean Combs, ‘P Diddy’, anakabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kingono kutoka kwa watu 120 wapya, wakiwemo wanaume 60 na wanawake 60.
Mawakili wanaowakilisha waathiriwa wanasema baadhi yao walikuwa watoto wakati wa matukio hayo huku mmoja akidai kuwa alinyanyaswa akiwa na umri wa miaka tisa.Tuhuma hizi zinaanzia mwaka 1991 hadi mwaka huu.
Tony Buzbee, wakili wa waathiriwa, alisema anatarajia kufungua kesi hizo ndani ya mwezi mmoja ujao, na kwamba sehemu kubwa ya mashtaka hayo yatapelekwa mahakamani kwenye majimbo ya New York na Los Angeles.
P Diddy tayari anakabiliwa na mashtaka mengine ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara ya ngono, ambapo alikana mashtaka hayo na kusema madai hayo ni ya uongo na ‘skendo’ za kumchafua.
Wakili wake wamesema baba huyo wa watoto saba atathibitisha kutokuwa na hatia mahakamani.
P Diddy amekuwa kizuizini tangu Septemba 17, 2024, baada ya kukana mashtaka ya kulazimisha wanawake kushiriki matukio ya kingono wakiwa wamelewa, pamoja na mashtaka mengine ya ulanguzi wa wanawake wanaojiuza na njama za ulaghai.
Mawakili wake wameomba dhamana ya dola milioni 50 ili awekwe chini ya ulinzi wa kifaa cha GPS akiwa nyumbani kwake Florida, lakini ombi hilo limekataliwa hadi sasa.
P Diddy alianzisha lebo ya Bad Boy Records mwaka 1993 na ni mmoja wa mabosi wakubwa kwenye tasnia ya muziki wa Hip Hop.