Mangungu, Hersi wateta fursa za AFCON 2027

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, na Rais wa Yanga, Hersi Said, wamewataka Watanzania kutumia fursa zitakazotokana na maandalizi na uenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Viongozi hao wamesema mashindano hayo yatakayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda ni nafasi kubwa kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa michezo kunufaika, hivyo wanapaswa kujiandaa mapema badala ya kusubiri kuelekezwa namna ya kutumia fursa hizo.
Akizungumza na SpotiLeo Dar es Salaam jana Mangungu amesema maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na kuipongeza Serikali kwa hatua inazochukua kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi na sekta binafsi kushiriki kikamilifu.
“AFCON ni fursa kubwa kwa Watanzania na hatupaswi kusubiri kuelekezwa namna ya kunufaika. Kila mmoja anapaswa kuangalia fursa zilizopo katika eneo lake na kuzitumia kiuchumi na kijamii. Tunapaswa kuhakikisha mashindano haya yanakuwa na manufaa kwa nchi yetu na wananchi kwa ujumla,” amesema Mangungu.
Akizungumzia uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuleta ofisi zake nchini, Mangungu amesema hatua hiyo ni ishara ya imani kwa Tanzania na inathibitisha kuwa nchi ina mazingira mazuri ya kupokea taasisi na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake, Hersi amesema uwepo wa ofisi za CAF nchini kuanzia Januari mwakani, ambazo zinatarajiwa kufanya kazi kwa zaidi ya miezi nane, utatoa fursa kwa Watanzania kupata ajira na kujifunza mifumo ya uendeshaji wa mashindano makubwa ya kimataifa.
Amesema nafasi mbalimbali za ajira zinatarajiwa kutangazwa na CAF, hivyo Watanzania wenye sifa wanapaswa kufuatilia matangazo hayo na kuomba ili wawe sehemu ya watakaoshiriki katika maandalizi na uendeshaji wa mashindano hayo.
Hersi ameongeza kuwa uwepo wa wataalamu wa CAF nchini utatoa nafasi kwa viongozi wa klabu na wadau wengine wa soka kupata uzoefu na kufahamu kwa karibu mifumo ya uendeshaji wa mashindano ya kimataifa.




