Mitindo

Warembo 24 kuingia kambini kuwania Miss Tanzania

DAR ES SALAAM: WAREMBO 24 wanatarajiwa kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya fainali za shindano la urembo la Miss Tanzania, linalotarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu katika viwanja vya Dar Village jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Habari Leo, Miss Tanzania 2026, Lea Lwendamseke maarufu Lamata, amesema maandalizi ya shindano hilo yatakuwa ya kipekee, huku mashabiki wakipata nafasi ya kufuatilia shughuli mbalimbali zitakazofanywa na washiriki wanapokuwa kambini.

Amesema washiriki hao wataonyesha shughuli zao za kila siku kupitia matangazo ya moja kwa moja (live), hatua itakayowapa mashabiki nafasi ya kufahamu kwa karibu maisha yao kambini, maandalizi na shughuli mbalimbali watakazoshiriki.

“Miss Tanzania itakuwa ya tofauti na miaka mingine yote. Mabinti hawa wana ndoto kubwa sana katika maisha yao, naamini kupitia shindano hili watatimiza ndoto zao,” amesema Lamata.

Amesema matarajio yake ni kuona shindano hilo likiwa jukwaa muhimu la kuwapa washiriki fursa ya kujifunza, kujitambua na kutumia vipaji vyao kufikia malengo waliyojiwekea.

Kuingia kambini kwa warembo hao 24 ni hatua muhimu kuelekea fainali ya shindano hilo, ambapo mmoja wao atatawazwa kuwa mshindi wa taji la Miss Tanzania.

Related Articles

Back to top button