Ligi Kuu

Simba yajichimbia Mbweni

DAR ES SALAAM: SIMBA wameingia kambini Mbweni, Dar es Salaam, kuanza maandalizi ya mwisho kuelekea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates utakaochezwa Jumapili.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu hiyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema wanaelekeza nguvu katika kuhakikisha wanakuwa tayari kwa mchezo huo muhimu.

“Tumeingia kambini Mbweni, ambapo wachezaji wanaendelea na programu maalumu ya mazoezi na maandalizi kuelekea mchezo wetu dhidi ya Orlando Pirates.

“Kwa taarifa tulizonazo, wageni wetu wanatarajiwa kuwasili Tanzania leo usiku, Novemba 26, na maandalizi yote ya kuwapokea yamekamilika. Kwa upande wetu tunaendelea kujipanga kuhakikisha tunakuwa tayari kwa mchezo huo muhimu,”amesema.

Kuhusu idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia Uwanja wa Uhuru, amesema taarifa ya awali iliyokuwepo ni mashabiki 6,000 pekee, lakini kuna matumaini ya idadi hiyo kuongezeka baada ya maboresho yaliyotakiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kukamilika kwa asilimia 100.

Amesema CAF ilifanya ukaguzi wa uwanja huo Novemba 25 na sasa klabu inasubiri majibu kuhusu idadi mpya ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia.

Ameongeza kuwa matumaini hayo pia yanatokana na juhudi za Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ambaye amekuwa akishughulikia suala hilo kwa kuishawishi CAF kuongeza idadi ya mashabiki kutoka 6,000 hadi 15,000.

Wakati wakisubiri uamuzi huo, Simba imeanza kuuza tiketi 6,000 zilizoruhusiwa awali, huku kiingilio kikiwa Sh 7,000 kwa mzunguko, Sh 40,000 VIP na Sh 200,000 Platinum.

Amewataka mashabiki wa Simba kutumia nafasi hiyo kununua tiketi mapema badala ya kusubiri uamuzi wa kuongeza idadi ya watazamaji, akieleza kuwa endapo ruhusa mpya itatolewa, tiketi nyingine zitaongezwa wakati mauzo yakiendelea.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button