Kusini Mwa Afrika

Dube aingia kinyang’anyiro cha mwanasoka bora Zimbabwe

HARARE: ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, ameweka jina lake katika orodha ya wachezaji 11 wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka 2026 nchini Zimbabwe, baada ya kutambuliwa kutokana na kiwango alichoonesha akiwa na klabu yake mpya ya Hardrock FC.

Hardrock imetangaza uteuzi huo ikijivunia kuwa na wachezaji watatu katika orodha hiyo, ambao ni Dube, mshambuliaji Washington Navaya na kiungo Neliswa Dlamini, kufuatia msimu mzuri ulioiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zimbabwe katika msimu wake wa kwanza tangu ipande daraja.

Dube, aliyejiunga na Hardrock Julai 2 mwaka huu akitokea Yanga, ameendelea kuthibitisha uwezo wake baada ya kuhusika katika mafanikio ya timu hiyo iliyomaliza msimu ikiwa na pointi 73 na kutwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Scottland FC.

Mshambuliaji huyo alikamilisha safari ya Hardrock kutwaa ubingwa kwa kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya FC Platinum Novemba 21, bao alilofunga dakika ya pili na kuipa klabu hiyo iliyopo Kwenye taji lake la kwanza la Ligi Kuu.

Uteuzi huo ni mwendelezo wa mafanikio ya Dube ambaye alitumia misimu miwili akiwa Yanga, akihusika katika mabao 37 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akifunga 13 na kutoa asisti nane msimu wa 2024/2025, kabla ya kufunga 10 na kutoa asisti sita msimu wa 2025/2026.

Kabla ya Yanga, Dube alitumikia Azam FC kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, ambapo msimu wake bora ulikuwa 2020/2021 alipofunga mabao 14 ya ligi, akimaliza miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na kiwango bora nchini.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Zimbabwe, orodha ya wachezaji 11 imechaguliwa kupitia mchakato uliowahusisha makocha, manahodha, waandishi wa habari na mashabiki, huku washindi wa nafasi tatu za juu wakitarajiwa kutangazwa katika hafla ya utoaji tuzo itakayofanyika Harare Desemba 4 mwaka huu.

Related Articles

Back to top button