Rais Samia atunukiwa tuzo, wasanii wagawiwa tozo

DAR ES SALAAM:RAIS Samia Suluhu Hassan ametunukiwa tuzo maalumu ya heshima kwa mchango wake katika kuanzisha tozo za hakimiliki zinazolenga kuhakikisha wasanii na wabunifu nchini wananufaika na matumizi ya kazi zao, huku wasanii wa muziki na filamu wakipokea mamilioni ya shilingi kupitia mgao huo.
Katika kundi la muziki, msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameongoza kwa kupata Sh milioni 12.2, akifuatiwa na Ali Saleh ‘Ali Kiba’ aliyepata Sh milioni 7.3, huku Kwaya ya Mtakatifu Cecilia ya Arusha ikishika nafasi ya tatu kwa kupata Sh milioni 6.8.
Kwa upande wa filamu, John Albert ameongoza kwa kupata Sh milioni 15, akifuatiwa na Hakimu Khatibu aliyepata Sh milioni 13, huku Empire Lokoma akishika nafasi ya tatu kwa kupata Sh milioni 11.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mapato hayo iliyofanyika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema Serikali itaendelea kusimamia na kulinda hakimiliki za wasanii ili wahakikishe wanapata stahiki zao kutokana na kazi wanazozalisha.
“Serikali itaendelea kusimamia maslahi ya wasanii. Hata hivyo, ni jukumu la wasanii kuhakikisha wanafanya kazi zenye ubora na zinazochangia kukuza uchumi wa nchi,” amesema.
Amesema wasanii wanapaswa kuongeza ubunifu, kuzingatia maadili ya Kitanzania na kusajili kazi zao COSOTA ili kurahisisha usimamizi na upatikanaji wa stahiki zao.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Naomi Mungure, amesema mfumo wa tozo za hakimiliki ulianzishwa kufuatia marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, kwa lengo la kulinda maslahi ya wabunifu.
Amesema katika awamu hiyo, mgao umetolewa kwa makundi matano ya ubunifu ambayo ni filamu, muziki, sanaa za ufundi, sanaa za maonesho na uandishi.




