Burudani

Bunge laahidi kutetea maslahi ya wasanii

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeahidi kuendelea kushirikiana na wasanii nchini katika kutetea maslahi yao na kusukuma mbele maboresho ya sheria na mifumo itakayowezesha wabunifu kunufaika na kazi zao.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Cornel Magembe aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati, Husna Sekiboko, katika hafla ya ugawaji wa tozo za hakimiliki kwa wasanii, waandishi na wabunifu iliyoandaliwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA).

Amesema ugawaji wa mirahaba unaofanyika ni matokeo ya marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge mwaka 2022, yaliyolenga kuweka mfumo utakaowezesha wasanii kupata manufaa kutokana na matumizi ya kazi zao.

“Naishukuru COSOTA kwa kuialika Kamati ya Bunge kushuhudia utekelezaji wa mfumo huo, hatua hiyo inaonesha matokeo ya kazi iliyofanywa na Bunge katika kutunga sheria zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, wakiwamo wasanii,”amesema.

Amesema marekebisho hayo yalitokana pia na maelekezo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa na dhamira ya kuhakikisha sekta ya sanaa inapata mazingira bora ya kukua na wabunifu wananufaika na kazi zao.

Ameeleza kuwa Kamati ya Bunge itaendelea kuwa sehemu ya kutetea maslahi ya wasanii kwa kupokea changamoto zao na kuzifikisha katika mamlaka husika, ikiwamo kuziwasilisha Bungeni ili zitafutiwe ufumbuzi kupitia taratibu zilizowekwa.

 

“Wasanii ni sehemu yetu na tutaendelea kusimama nao pamoja. Mambo yoyote mtakayokuwa nayo na kuhitaji msaada wetu tutayabeba kama ya kwetu na kuyafikisha kwenye mamlaka husika ili yaweze kufanyiwa kazi,” amesema.

Amesema kamati hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa sanaa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika kushughulikia changamoto zao, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Bunge, COSOTA na taasisi nyingine zinazohusika na maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, amewapongeza viongozi na bodi ya COSOTA kwa kuandaa hafla hiyo, akisema kamati itaendelea kutekeleza jukumu lake la kusikiliza na kufuatilia kero za wasanii ili kuhakikisha zinapata ufumbuzi.

Related Articles

Back to top button