Mastaa

Wasanii wajitokeza kupimwa moyo bure JKCI

DAR ES SALAAM: WASANII mbalimbali wakiongozwa na  Mboso Khan na Zuhura Othuman ‘Zuchu’ wamejitokeza kupima moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi la Kawe jengo la Benjamini Mkapa.

Akizungumza na Habari leo wakati wakiendelea na zoezi la upimaji moyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo, Dk Peter Kisenge amesema kuwa wanaendelea kupima wasanii wa tasnia mbalimbali na hivyo amesisitiza wajitokeze.

“Niwaombe wasanii ambao bado hawajajitokeza kupima wajitokeze na wapime ili waishi wakiwa wanazijua afya zao na kuendelea kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi. Tulianza na wachezaji mpira na sasa hivi tupo na wasanii ambapo tukimaliza tutatangaza kundi lingine litakalofuata kupima na kuangalia kama wana matatizo ya moyo. Lengo ni kuwasaidia wasanii wasiwe na magonjwa yasiyoambukiza lakini pia wawe na kawaida ya kupima afya zao na kuendelea vizuri na majukumu yao ya kila siku katika kuelimisha na kuburudisha jamii,”amesema  Dk Kisenge.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini Gervas Kasiga ‘Chuma’ amesema kuwa huduma hiyo ya upimaji itaendelea kuwepo kwa siku za jumamosi na jumapili hadi Januari 2025.

“Tunafurahi kuona wasanii wanaendelea kujitokeza kwa wingi kupima moyo. Hili ni jambo zuri lakini nitoe wito kwa wengine ambao hawajajitokeza waje kupima na kujua afya zao kama wana tatizo ama hawana,” amesema Kasiga.

Aidha Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Kedmon Mapana ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Taasisi ya ‘Mama ongea na mwanao’  ambao kwa pamoja wameweza kufanikisha jambo hili.

Naye Mboso Khan ameishukuru serikali kwa kutoa matibabu ya moyo kwa Wasanii ambapoa mesema kwamba yeye binafsi amekutwa na ugonjwa wa moyo na ameanza rasmi matibabu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button