Timu za taifa zapata udhamini wa vinywaji

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesaini mkataba mkubwa wa udhamini wa miaka miwili na kampuni ya Watercom Tanzania.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, Rais wa TFF Wallace Karia na Meneja Masoko wa Watercom Mohamed Salim walisaini makubaliano yanayohusisha udhamini wa vinywaji rasmi vitakavyotumika katika programu zote za timu za taifa ikiwemo maji safi ya kunywa na juisi za kuongeza nguvu.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Watercom itahakikisha timu zote za taifa zikiwemo Serengeti Boys, Twiga Stars, Taifa Stars na timu nyingine kwenye ngazi mbalimbali zinapata huduma bora za vinywaji wakati wa kambi, mazoezi na michezo ya kimataifa.
Akizungumza baada ya kusaini, Rais wa TFF Karia amesema kuwa udhamini huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa wachezaji na kuongeza ufanisi wa maandalizi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na michezo.
Kwa upande wake, Mohamed Salim wa Watercom alieleza kuwa kampuni yao imejipanga kuunga mkono juhudi za kuibua na kuendeleza vipaji nchini, na kwamba udhamini huo ni ishara ya uzalendo na dhamira yao ya kuendeleza michezo Tanzania.




