Bravos Yaendelea kuvuruga vichwa Coastal Union
DAR ES SALAAM: BAADA ya kichapo cha bao 3-0 kutoka kwa Bravos ya Angola timu ya Coastal Union imewataka wachezaji waweke akilini kwamba lazima mechi ya marudiano waweke historia ya kuvuka hatua ya awali kwa kushinda bao zaidi ya nne na kama kuna mchezaji aamini katika hilo hafai kwenye timu hiyo.
Meneja wa habari wa Coastal Abbas el Sabri amesema hayo kupitia kituo kimoja cha redio nchini akidai kwamba wameshazungumza na wachezaji na wamewaambia kama kuna mchezaji asiyeamini katika kupindua matokeo aachane na timu hiyo akatafute timu nyinyine.
“Lengo letu tunataka kila mchezaji ajitambue kwamba yeye ni sehemu ya ushindi wa kihistoria tutakaouweka katika mechi ya marudiano dhidi ya Bravo ya Angola na hilo tuliliweka wazi kwa wachezaji wote mbele ya balozi wetu nchini Angpla baada tu ya kumaliza mchezo tuliopigwa 3-0” alifafanua meneja huyo wa habari.
Sabri alisema leo Jumanne wataweka kikao kizito na wazee wa timu hiyo ili kupanga harakati za ushindi kuanzia nje ya uwanja hadi ndani.
“Tuna kikao kizito na wazee wetu pia tutazungumza na mashabiki wetu ili kuwafanya Bravos wakija nchini waone wapo ugenini hadi watakaporudi kwao kama sisi tulivyokuwa kwao,” alisema Sabri.
Sabri alisema malengo ya Coastal Union ni kufika hatua ya makundi na wanaimani kwa muitikio wa wachezaji wao, wazee na mashabiki wataweka historia kubwa ya kuvuka kwa zaidi ya 3.
“Tunaamini tutapindua mechi kwa kupata magoli matatu bila kisha tutaongeza moja sisi hao tunaenda Congo kuendelea na mashindano,” alisema.