
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ndiye mgeni rasmi katika ufunguzi wa Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (Shimiwi) utakaofanyika Oktoka 20 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Katibu Mkuu wa Shimiwi, Moshi Makuka alisema jana kuwa mashindano hayo, ambayo yatashindanisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, riadha, baiskeli, karata, drafti na bao yatamalizika Novemba 2, 2021.
Makuka alisema kuwa michezo ya soka, netiboli na kamba itachezwa kwa mtindo wa ligi na zitakapofika hatua ya 32 bora, timu hizo zitaanza hatua ya mtoano hadi fainali.
Alisema kuwa tayari timu 23 za wizara, mikoa 12 na Idara tisa zinazojitegemea zimethibitisha kushiriki michezo hiyo, ambayo kwa mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2014.
Alisema kuwa mbali na Uwanja wa Jamhuri, ambao utatumika kufungulia na kufungia michezo hiyo, viwanja vingine vitakavyotumika kuchezea michezo mbalimbali ni Mazimbu, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Tumbaku na Sekondari ya Morogoro.
Aidha, Makuka amezitaka timu zote kuthibitisha ushiriki wao pamoja na michezo watakayoshiriki ili ratiba zipangwe mapema na kujua idadi ya timu shiriki mwaka huu.
Akizungumzia ufungaji, alisema michezo ya mwaka huu inatarajia kufungwa Novemba 2 na Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Hussein Kattanga.