TETESI ZA USAJILI ULAYA
Real Madrid yamvuruga Trent
HATMA ya Trent Alexander-Arnold klabuni Liverpool ipo mashakani baada ya mazungumzo ya hivi karibuni kati ya mchezaji huyo na klabu ya Real Madrid. Mkataba wa Trent pale Anfield unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu na hakuna dalili yoyote kwa mchezaji huyo mwenye miaka 25 kusaini mkataba mpya wa kendelea kubaki klabuni hapo.
Taarifa zinaeleza kwamba klabu hiyo inavizia nafasi ya kumchukua Trent bure pindi mkataba wake utakapokamilika na pia inasemekana kwamba mchezaji huyo amekataa ofa ya Liverpool ya kusaini kandarasi mpya. Kuumia kwa Carvajal katika mchezo wa juzi dhidi ya Villareal kunaweza kuilazimu klabu hiyo kusaka beki mpya wa kulia haraka iwezekanavyo lakini bado chaguo la kwanza ni kwa Trent.
PSG yasuka mtego wa Salah
KLABU ya Liverpool inaweza kumpoteza winga Mohammed Salah ambaye anatarajia kujiunga na Paris Saint- Germain (PSG). Wababe hao wa Ligue 1 wanaongoza mbio za kumuwania mchezaji huyo ambaye ni tegemezi kwa Majogoo wa Jiji la Liverpool.
Salah, 32, anamalizia miezi ya mwisho ya mkataba wake klabuni hapo kwani mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu na licha ya klabu kadhaa kutoka Saudi Arabia kuhitaji huduma yake, imeelezwa kwamba PSG imeandaa dau nono kwa mchezaji huyo ili aendelee kusalia barani Ulaya. The Sun inaeleza kuwa PSG iko tayari kumpa ofa Salah ya kuitumikia klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.
Xabi Alonso kumrithi Ten Hag United
TAARIFA zinaeleza kwamba Klabu ya Manchester United iko tayari kusubiri hadi majira yajayo ya kiangazi ili kumnasa nguli wa zamani wa Liverpool na kocha wa sasa wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso ili kuziba nafasi itakayoachwa wazi na Erik ten Hag pindi atakapoondoka klabuni hapo.
Nafasi ya Ten Hag klabuni hapo imekuwa ya mashaka kwa mara nyingine tena kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo ya kikosi hicho hali inayopelekea mabosi wa klabu hiyo kuanza kuangalia uwezekano wa kupata mbadala atakayekuja kuleta matumaini mapya ya klabu. Katika michezo 10 iliyopita United imeshinda michezo mitatu tu huku mchezo wa mwisho walioshinda ukiwa ni 7-0 dhidi ya Barnsley septemba 17, 2024.
Sambamba na Alonso, taarifa zinaeleza kwamba mabosi hao wanawatazama kwa karibu makocha wengine kama Ruud Van Nistelrooy, Eddie Howe, Gareth Southgate, Thomas Tuchel, Max Allegri na Graham Potter.
Ronaldo amtaka De Bryune
WASIWASI umewakumba mashabaki wa Manchester City baada ya taarifa kuenea kwamba nahodha wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo amewashawishi mabosi wa klabu hiyo ya Saudi Arabia kujaribu kumsaini Kevin De Bruyne msimu unaokuja.
Inaripotiwa kwamba Al-Nassr inaweza kumpa ofa KDB ya mshahara wa pauni milioni 1 kwa wiki,kitu ambacho kitakuwa ni ngumu kwa De Bruyne kukataa. CR7 anamuona De Bruyne kama usajili ambao utakuja kuibadili Al-Nassr kwani mpaka sasa Ronaldo hajabeba kombe lolote kubwa na klabu hiyo.
De Bryune,33, amehudumu EPL kwa takribani misimu 10 sasa, akiifungia Manchester City mabao 103, na kutoa pasi 171 za mabao.
Vigogo EPL kumuwania Marmoush
ARSENAL, Liverpool na Mancheter United wameonesha kuvutiwa na huduma ya mshambuliaji klabu ya Eintracht Frankfurt, Omar Marmoush. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri ameanza vyema msimu huu akifunga mabao 6 kwenye michezo mitano tu katika michuano yote.
Klabu zote hizo zina washambuliaji wake wazuri tayari, lakini wanaangalia namna ya kuongeza upana wa kikosi katika eneo la ushambuliaji. Taarifa zinaeleza kwamba Marmoush,25, anaweza kuondoka klabuni hapo endapo klabu hizo zitatoa dau linalokaribia Euro milioni 30.
Sambamba na timu hizo, West Ham na Nottingham Forest ni klabu zinamuangalia kwa karibu pia mchezaji huyo.
Chelsea yavutiwa na Adeyemi
CHELSEA imeonesha nia ya kutaka kumsajili winga mwenye kasi wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi. Klabu hiyo yenye maskani yake jijini London inatafuta mchezaji mwingine wa nafasi ya pembeni na tayari jicho lake limetua kwa Adeyemi mwenye miaka 22.
Imeelezwa kwamba kocha wa Chelsea, Enzo Maresca anahitaji huduma ya mshambuliaji huyo ambaye dau lake sokoni linakadiriwa kuwa ni Euro milioni 50.