Wasanii, viongozi waomboleza kifo Hashim Kambi

DAR ES SALAAM- MWILI wa msanii mkongwe wa tasnia ya uigizaji, Hashim Kambi, uliagwa jana katika Msikiti wa Maamur jijini Dar es Salaam kabla ya kuzikwa katika makaburi ya Kisutu, huku wasanii, viongozi na wadau wa sanaa wakijitokeza kutoa heshima zao za mwisho.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal maarufu Sheta, amesema kifo hicho ni funzo kwa jamii, hususan wasanii, kuishi kwa upendo na mshikamano.
“Kwa niaba ya Jiji, tunatoa pole. Rais Samia Suluhu Hassan pia ametuma salamu za rambirambi. Msiba huu utufundishe kupendana na kuepuka migogoro isiyo ya lazima,” amesema.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Waislamu wa Dar es Salaam, Sheikh Mkuu wa mkoa huo, Walid Alhad Omar, amesema msiba huo ni ukumbusho wa maisha ya mwanadamu kuwa ya muda mfupi duniani.

“Haya ndiyo maisha, Mtume anasema ishi utakavyoishi lakini ujue ipo siku utaiacha dunia. Misiba kama hii inatukumbusha kuwa tutarudi kwa Mwenyezi Mungu kwa maisha ya hakika,” amesema.
Kwa upande wa tasnia, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Gervas Kasiga amewataka wanatasnia kuendeleza mshikamano na kuthamini utu, wakitumia mfano wa mazuri aliyofanya Kambi katika tasnia hiyo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Rajabu Amir, amesema tasnia imepoteza mtu muhimu na kuwataka wasanii kuyaishi mema aliyoyaacha marehemu.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengele, amesema kifo hakiwezi kuzoeleka, akitoa wito kwa familia kushikamana katika kipindi hiki cha majonzi.
“Watoto na familia kwa ujumla huu ni muda wa kuungana na kumuenzi mzee wenu. Sisi tumekabidhiwa milioni tano na kuongeza milioni mbili ili kuishika mkono familia,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Azam Media, Baruan Muhuza, amesema kifo cha Kambi kimeacha pengo kubwa kwa wadau wa tasnia hiyo, akieleza kuwa pamoja na kuigiza, marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika uingizaji wa sauti kwenye tamthilia mbalimbali.
“Tumepata mshtuko mkubwa baada ya taarifa hizi. Ni kweli ameondoka duniani, lakini kazi zake zinaendelea kuishi. Tunaungana na familia yake katika kipindi hiki kigumu,” amesema.
Akizungumza kwa hisia, mwigizaji mwenzake Mzee Chilo amesema marehemu alikuwa mtu wa karibu kwake katika mambo mengi ya kheri, akisisitiza kuwa kifo ni ukumbusho kwa wanadamu wote.
“Tumepoteza mtu muhimu, lakini Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwamba sote tutaondoka hapa duniani. Tumuombee apokelewe na mola wake, na mema yake ndiyo yatakayobaki kukumbukwa,” amesema.
Kambi alifariki juzi kwa maradhi ya presha na jana amezikwa.



