Barca yajiandaa vita kumwania Haaland

MIAMBA ya Hispania, Barcelona inajiandaa katika vita kupigania saini ya nyota wa Manchester City, Erling Haaland.
Kwa muda mrefu Real Madrid imekuwa ikichukuliwa kama timu inayomfaa zaidi Haaland, lakini sasa kwa mujibu wa tovuti ya michezo 90min, Barca inajiandaa kufanya harakati kumsajili mshambuliaji huyo mahiri raia wa Norway.
Kwa sasa Barca ina Robert Lewandowski anayeongoza safu ya ushambuliaji Lakini katika mpango wa muda mrefu, Haaland anaonekana chaguo linalofaa kuwa mbadala wa mkongwe huyo wa Poland, ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 35.
Mapema mwezi huu ripoti zilisema Manchester City inapanga kumpatia Haaland ofa ya pauni 600,000 sawa na shilingi bilioni 1.84 kwa wiki ikihofia huenda akarubuniwa ahamie klabu za Saudi Arabia au Read Madrid.
Haaland ameng’ara Manchester City tangu alipowasili msimu uliopita akitokea Borussia Dortmund kwa mkataba wa miaka mitano akisaidia klabu hiyo ya Manchester kutwaa mataji matatu likiwemo Ligi ya Mabingwa huku akishinda kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu England na cha Ulaya.
Kwa jumla Haaland mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao 52 katika mashindano yote yakiwemo 36 aliyoweka rekodi EPL.