Kwingineko

Bayern yaiwinda PSG kwa kisasi baada ya kipigo cha mabao tisa

MUNICH:KLABU ya Bayern Munich imeweka wazi dhamira ya kulipa kisasi dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya UEFA Champions League baada ya kupoteza kwa mabao 5-4 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Ufaransa.

Mchezo huo uliingia kwenye rekodi kwa kuwa na mabao mengi zaidi katika hatua ya nusu fainali, huku timu zote zikionesha soka la kushambulia lililowavutia mashabiki duniani.

Kocha wa Bayern, Vincent Kompany amesema mashabiki wanapaswa kutarajia burudani zaidi katika mchezo wa marudiano, akisisitiza kuwa timu yake haitaridhika na matokeo ya kwanza.

“Zaidi… tunataka zaidi. Tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki 75,000, hatutaki kelele tu bali nguvu kubwa ya sapoti,” alisema Kompany.

Bayern imekuwa katika kiwango cha juu msimu huu baada ya kuvunja rekodi ya kufunga mabao mengi katika ligi ya Ujerumani, ikiwa imefikisha mabao 113 huku mechi tatu zikiwa zimesalia, rekodi iliyopita ilikuwa mabao 101 yaliyowekwa tangu msimu wa 1971/72.

Katika UEFA Champions League msimu huu, Bayern pia imeweka historia kwa kuwa na wachezaji watatu – Harry Kane, Michael Olise na Luis Diaz – waliohusika na mabao 10 au zaidi (kufunga na kutoa pasi za mabao).

Nahodha huyo wa England, Kane, anaongoza kwa mabao 13 katika michuano hiyo na pia ndiye kinara wa mabao katika Bundesliga akiwa na mabao 33.

Licha ya kuruhusu mabao matano katika mchezo wa kwanza, Kompany anaamini bado wana nafasi kubwa ya kusonga mbele.

“Unapofungwa mabao matano Champions League unaonekana kama umetoka, lakini sisi tulifunga manne ugenini. Tuna uwezo wa kufunga na tutafanya hivyo tena nyumbani,” alisisitiza.

Bayern sasa italazimika kushinda nyumbani ili kufufua matumaini ya kutinga fainali, huku mashabiki wao wakitajwa kuwa silaha muhimu katika vita hiyo kali dhidi ya mabingwa watetezi PSG.

Related Articles

Back to top button