AFCONAfrica

Tanzania kuomba uenyeji AFCON 2027

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kupitia Pamoja Bid zimedhamiria kuwa mwenyeji wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON) 2027.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Dodoma Rais Samia amesema nchi hizo zinawania nafasi hiyo kwa kutambua mafanikio makubwa ambayo sekta ya michezo imepata hivyo kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kutaongeza hamasa zaidi kwa ukuaji wa michezo hususan soka.

“Michuano hii itachangia katika ukuaji wa utalii kwa kuwa ni mashindano ambayo hutazamwa na zaidi ya watu bilioni moja barani Afrika na maeneo mengine duniani kwa ujumla,”amesema Rais Samia katika taarifa hiyo.

Amesema mashindano hayo yatawezesha na kunufaisha sekta nyingi za uchumi nchini ambazo huchangia ajira, mapato kwa wafanyabiashara na serikali.

Kwa upande mwingine mkuu huyo wa nchi amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) imefanya utafiti na kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Iwapo Tanzania, Kenya na Uganda zitakubaliwa kuandaa AFCON 2027, itakuwa mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki tangu yaanzishwe mwaka 1957.

Related Articles

Back to top button