Africa

Simba, Yanga zinapooga manoti kuitafuta robo fainali

TANZANIA imeendelea kuwa kwenye mikono salama kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu za Simba na Yanga zikiendelea kuipeperusha
bendera ya nchi.

Huwezi kulitaja soka la Tanzania bila kuitaja klabu ya Simba, ambayo inaipeperusha vyema bendera ya taifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Simba wako Kundi C wakiwa nafasi ya tatu na pointi tatu baada ya michezo mitatu wakishinda mchezo mmoja na kupoteza miwili, ikihitaji ushindi kwenye michezo iliyosalia ili kutafuta nafasi ya kutinga
hatua ya robo fainali.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Yanga imeendelea kuiwakilisha vema Tanzania ikiwa Kundi D,
ikishika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja sare moja na kupoteza mara moja.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamekuwa tishio zaidi sio hapa  yumbani pekee, bali Afrika ambako hivi sasa ndio timu ambayo imekuwa gumzo zaidi kutokana na kuwa katika kiwango cha juu na kuwa tishio kwa klabu kubwa kutokana na ubora wao wa nje na ndani ya uwanja.

Wiki ijayo timu hizi shiriki kwenye michuano ya Caf zinaenda kurusha karata zao kwenye  igi ya Mabingwa Simba watakuwa wenyeji wa Vipers kutoka Uganda wakati Yanga kwenye
Kombe la Shirikisho Afrika wao watawakaribisha AS Real Bamako ya Mali.

MECHI YA MAHESABU
Simba inahitaji ushindi dhidi ya Vipers ili kufufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuanza kwa kuchechemea kwa kupata vipigo viwili katika mechi mbili za awali.

Ushindi utaifanya kufikisha pointi sita wakati huo wakiiombea Raja Casablanca ishinde mchezo wake wa ugenini dhidi ya Horoya ili kuisimamisha timu hiyo ya Guinea ambayo ndio tishio kwa Simba.

Yanga wao baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 itakuwa ikitafuta pointi tatu zitakazowasogeza juu ya msimamo wa kundi D baada ya kushinda mchezo mmoja, sare na kupoteza mara moja.

Ushindi utaifanya ifikishe pointi saba huku ikiiombea TP Mazembe iifunge US Monastir
ambayo ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo ikishinda mara mbili na sare moja.

MANOTI KUONGEZAMORALI YA TIMU
Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuongeza chachu kwa timu hizi baada ya kuahidi kutoa milioni tano kwa kila bao, lakini sasa neema zimeendelea kumiminika baada ya wadau wengine kumuunga mkono na sasa bao moja kufikia Sh milioni 11.

Lengo ni kuwafanya wachezaji waongeze ari ya kupambana na kuipeperusha bendera ya Tanzania, ambapo hadi sasa Yanga imechukua Sh milioni 20 kutoka kwenye ahadi ya Rais
Samia Suluhu Hassan wakati Simba wakipokea Sh milioni 5 pekee.

Yanga ilichukua Sh milioni 15 kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Sh milioni tano baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na
AS Real Bamako nchini Mali.

Simba wao walikusanya Sh milioni tano kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers kwenye Uwanja wa St Mary’s Kitende jijini Kampala nchini Uganda.

Mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri.

MAYELE, PHIRI WAVISHWA MABOMU
Miongoni mwa nyota ambao macho ya mashabiki wa soka na imani juu yao ni Fiston Mayele kinara wa mabao kwenye kikosi cha Yanga ambaye hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara amepachika mabao 15.

Mayele pia tayari amefungua akaunti ya mabao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuisaidia timu yake kuondoka na pointi moja baada ya kuilazimisha sare AS Real Bamako ya Mali.

Hadi sasa Mayele ameichangia Yanga mabao mawili, akifunga moja na kutoa pasi moja ya bao. Simba wao matumaini yao yako chini ya mshambuliaji, Moses Phiri, ambaye ndio mshambuliaji kinara kwenye jeshi la Roberto akiwa na mabao 10 kwenye Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo alikuwa na mwanzo mzuri kwenye michezo ya kufuzu hatua ya makundi kwa kupachika mabao manne lakini majeraha yalimrudisha nyuma akaikosa michezo miwili ya awali na sasa amerejea.

Katika mchezo wake wa kwanza tayari amechangia bao moja kwa kutoa pasi ya bao kwa Henock Inonga katika mchezo ambao Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers.

REKODI ZAO KUWABEBA
Kwa sasa Simba ndio klabu pekee katika ukanda huu wa Afrika Mashariki yenye rekodi ya kucheza hatua ya makundi mara tatu ndani ya miaka mitano ikifanya hivyo katika misimu ya 2018/19 chini ya kocha Patrick Aussems, 2020/21 chini ya Didier Gomes na 2022/23 chini ya Juma Mgunda.

Hizi ni baadhi ya rekodi zilizowekwa na klabu ya Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu wa mwaka 2022/23 na kuwa gumzo kila kona ya Afrika Mashariki. Wakati Yanga wao wameendelea kuweka rekodi ya kuwa timu iliyofika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mara nyingi zaidi.

Yanga imefika hatua ya makundi mara tatu mwaka 2016/17 chini ya Hans van der Pluijm,
mwaka 2018/19 chini ya George Lwandamina na mwaka 2022/23 chini ya Nasreddine Nabi.

LIGI KUU BARA YAENDELEA KUPAA
Simba imeendelea kuwa na mfululizo wa wachezaji bora wa wiki katika hatua ya makundi baada ya beki wa kati Henock Inonga kuwemo katika orodha ya wachezaji bora wa wiki wa
Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwenye Kombe la Shirikisho straika mpya wa Yanga, Kennedy Musonda amekuwa nyota wa kwanza kuingia kwenye kikosi bora cha wiki cha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Nyota hao hawajapenya hivi hivi katika vikosi bora vya wiki, Inonga ameingia baada ya kuipa bao la ushindi timu yake wakati Musonda yeye aliisaidia Yanga kupata ushindi wa
mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe.

Related Articles

Back to top button